Habari za Punde

*TASWA FC KUKIPIGA NA WAANDISHI WA NJE

TIMU inayoundwa na waandishi wa Habari za Michezo Tanzania, TASWA Fc, inatarajia kucheza mchezo wa kirafiki na timu mchanganyiko itakayoundwa na waandishi wa habari za michezo waliofika nchini kuripoti mashindano ya Challenge.

Akizungumza na gazeti hili Mwenyekiti wa Taswa Fc, Majuto Omary, alisema kuwa maandalizi ya mchezo huo yanaendelea na tayari yameshafanyika mazungumzo baina ya viongozi wa timu hizi mbili na kufikia makubaliano.

Aidha alisema kuwa waandishi hao wa nje wamefikia uamuzi huo baada ya kupata taarifa za timu ya Taswa jinsi inavyoshiriki na kufanya vizuri katika michezo na hasa mpira wa miguu.

“Kama mnavyojua jamani waandishi wa habari za michezo ambao hupenda soka, siku zote wanaposafiri hawaachi vifaa vya michezo hata iwe amesafiri mkoani ama nje ya nchi ili aweze kufanya hata mazoezi ya kujiweka sawa tu,

Hivyo hata hawa waandishi wenzetu wapo kamili na kila mmoja wao ana vifaa vyake vya michezo na wamevutiwa na timu yetu inavyofanya vizuri na ndiyo maana wamethubutu kutaka mech ya kirafiki nasi”, alisema Majuto.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa hivi karibuni ambapo bado viongozi wa timu hizo wanafanya mazungumzo na waandaaji wa michuano ya Challenge, ili kuweza kuona uwezekano wa kucheza kama mchezo wa utangulizi katika moja ya mchezo wa hatua ya robo fainali katika Uwanja wa Taifa.

Alisema kuwa iwapo itashindikana kupata nafasi ya aina hiyo, basi mchezo huo utaandaliwa katika uwanja wa Chuo cha Posta, ambapo unaweza kuchezwa siku ya mapumziko ya michuano hiyo ya Challenge.

Baadhi ya wachezaji wanaounda Kikosi cha Taswa Fc, ni walimu wa timu hiyo, Ibrahim Maestro na Ally Mkongwe, Majuto Omary, Salleh Ally, Muhidin Sufiani, Mbozi Ernest, Ellius Kambili, Shadrack Killas, Willbroad Moland, Juma Mohamed.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.