Rais Kikwete amesema hayo leo katika sherehe ya kukabidhiwa shule ya Msingi ya Msoga na kaimu balozi wa China nchini Tanzania bw. Fu Jijun,
" Wazazi tuanze kuzungumzia suala la watoto wetu kupata chakula shuleni, watoto wakipata uji watafaulu zaidi haya tunayaweza'
Rais Kikwete ametoa changamoto hiyo kwa wazazi na wanakijiji wenzie wa Msoga baada ya kukabidhiwa shule ya Msingi Msoga iliyojengwa na serikali ya China kufuatia ahadi ya serikali ya China, chini ya Mpango wa Ushirikiano baina ya China na Afrika.
Katika ushirikiano baina ya china na Africa nchi 48 zitapata jumla ya shule 100 za msingi na Tanzania imepata shule tatu ambazo ni Msoga, Kiteto na ingine itajengwa visiwani Zanzibar.
Balozi Jijun amesema katika kipindi cha miaka mitatu ijayo Tanzania itapata shule zingine tatu katika maeneo tofauti hapa nchini.
Shule ya Msoga imejengwa katika kijiji cha Msoga ambapo awali katika miaka ya nyuma palikua na shule ya msingi ambayo Rais Kikwete alisoma darasa la kwanza hadi la nne.
Baadae shule hiyo pamoja na zahanati na jengo la mahakama kijijini hapo vilibomolewa kwa ajili ya kupisha maendeleo.
Rais Kikwete amehudhuria sherehe hiyo kama mmoja wa wana kijiji na mwana jamii wa Msoga.
Mara kwa mara Rais Kikwete hutembelea kijijini kwake mwishoni mwa wiki ama wakati wa likizo na sherehe mbalimbali ambapo hujumuika kikamilifu katika shughuli za kujadili na kupanga maendeleo ya wana Msoga.
Rais amewataka wana Msoga waanze kufikiria namna ya kujenga nyumba bora, ufugaji wa kuku na kilimo bora ili waweze kuinua hali zao za maisha na za watoto wao
"Tukae tufanye uamuzi wa busara, tupange mazao yenye thamani, mbogamboga na ufugaji bora na wa kisasa, tukifanya hivyo hatutashindwa kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wetu" amesisitiza
Rais ameishukuru serikali ya China kwa msaada hu na kuelezea uhusiano baina ya Tanzania na China kuwa ni uhusiano wa wakati wote (all weather friendship), na kueleza kuwa Tanzania imefaidika sana na urafiki huo.
Balozi Jijun ametoa zawadi ya Computer 3 za mezani na mipira 20 ya kuchezea watoto na Rais akatoa zawadi ya computer 2 na televisheni 2
Imetolewa na PK.
No comments:
Post a Comment