Na Francis Godwin, Iringa
POLISI mkoani Iringa wanadaiwa kutenda unyama baada ya askari kanzu wa kike wa Jeshi la Polisi mkoani humo, kumtwanga risasi ya mguu mfanyabiashara ndogo ndogo, Frida Mgima (33) mkazi wa Iringa wakati akiteremka katika gari dogo la kukodi (taksi) nje ya baa moja maarufu.
Tukio hilo la kinyama lilitokea Februari 4 mwaka huu majira ya saa 11 za jioni wakati mfanyabiashara huyo akiwa anashuka katika gari hilo aina ya Ballon lenye namba T 450 AEA, akiingia kwenye baa hiyo kwa ajili ya kununua chips.
Akizungumzia tukio hilo nyumbani kwake maeneo ya Don Bosco, alisema kuwa . akiuguza jeraha hilo baada ya kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa,Frida alisema kuwa hakujua alipigwa risasi hiyo na askari huyo kwa lengo gani.
Alisema muda mfupi baada ya tukio hilo alifuatwa na kusindikizwa na askari waliokuwa doria karibu na baa hiyo na kwenda kituo kikuu cha Polisi Wilaya ya Iringa kupewa kibali cha kupata matibabu (PF3).
Alisema baada ya kufika kituoni na kupewa PF3 alikwenda kutibiwa katika Hospitali ya mkoa wa Iringa ingawa wakati wa tukio hilo hakuelezwa na mtuhumiwa huyo (askari kanzu wa kike) alipigwa risasi hiyo kwa kosa gani.
Katika tukio hilo, mfanyabiashara huyo akiwa na mwanae wa miaka tisa (9) Miki, amedai alipoteza fedha za makusanyo ya biashara zake kiasi cha sh. 500,000 pamoja na simu ya mkononi.
“Nikiitwa katika gwaride la utambulisho nitawaonyesha, yule askari ni wa upelelezi mimi namjua, alikuwa amevaa koti na amebeba redio call ya Polisi, alinitwanga shaba mguu wa kushoto lakini namshukuru Mungu hakuniua nimepona…sijui nimefanyiwa hivi kwa kosa gani”,alihoji mwanamke huyo huku akiangua kilio.
Hata hivyo,Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa Evarist Mangala alipotafutwa kuzungumzia sakata hili, alisema kuwa hana taarifa ya tukio hilo na kwamba askari wa kike hawaruhusiwi kubeba silaha.
“Nimewasiliana na OCD wangu tukio kama hilo halipo na halina ukweli wowote…askari wa kike hawaruhusiwi kubeba silaha,huyo aliyemuona alipata wapi hiyo silaha anayosema…ndugu yangu hakuna ukweli katika tukio hilo”,alisema Kamanda Mangala.
No comments:
Post a Comment