Habari za Punde

*KAMPUNI YA MAFUTA YA MDAULA YA SONGEA YAIPIGA JEKI TIMU YA MAJIMAJI

Na Beatrice Mlyansi-MAELEZO
KAMPUNI ya mafuta ya Mdaula ya mjini Songea, leo imetoa mchango wa shilingi milioni kumi (10,000,000/=) kusaidia timu ya mpira wa miguu ya Majimaji ya Songea inayoshiriki ligi kuu ya Vodacom nchini.
Akizungumza jijini Dar es salaam baada ya kutoa mchango huo, Mwakilishi wa Kampuni ya Mdaula, Hafidh Hashim, amesema, kampuni yake imeamua kutoa mchango huo ili kuiwezesha timu ya Majimaji kufanya maandalizi yatakayoiwezesha kufanya vizuri katika mashindano ya ligi kuu ya Vodacom yanayoendelea na pia kujiandaa kwa ligi hiyo katika msimu ujao
.Amesema, wachezaji wanahitaji huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja gharama za usafiri, posho na malazi.
“Sisi kama wafanyabiashara tunaona ni vizuri kusaidia timu hii ambayo inawakilisha mkoa wa Ruvuma na wananchi wake, Hivyo basi inahitaji kupewa msaada wa hali na mali,
Naye Mjumbe wa Kamati ya Uwezeshaji wa timu hiyo, John Nchimbi, amesema, timu ya Majimaji iliomba msaada kwa wadau mbalimbali kuisaidia iweze kujiendesha badala ya kutegemea mapato yanayotokana na viingilio vya milangoni.
“tunashukuru kwa msaada tulioupata, kwani tuliomba wadau mbalimbali na Mdaula ndio pekee waliojitokeza mpaka sasa.” Alisema Nchimbi.
Msemaji wa Timu ya Majimaji , Steven Ndauka, amesema, mchango walioupata ni mkubwa na utaisaidia timu ya hiyo katika kutatua baadhi ya mambo.
Aliishukuru Kampuni hiyo ya Mdaula kwa kuitikia wito wa kusaidia michezo katika mkoa wa Ruvuma, hususan timu ya Majimaji. Aidha, ametoa wito kwa kampuni nyingine kujitokeza kusaidia timu za mikoani.
Kampuni ya Mdaula ni Moja ya Makampuni makubwa ya mafuta mkoani Ruvuma na imekuwa ikijitoa kusaidia michezo mara kwa mara.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.