Habari za Punde

RAIS JAKAYA KIKWETE AFANYA ZIARA WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA NA WATOTO

Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii jinsia na Watoto wakati wa ziara yake ya kikazi wizarani hapo leo mchana.Wapili kulia ni Waziri wa wizara hiyo Bi.Sophia Simba. picha na freddy

Maro


HOTUBA YA WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA NA WATOTO MHESHIMIWA SOFIA SIMBA ILIYOTOLEWA KWA MHESHIMIWA RAIS JAKAYA MRISHO KIKWETE KATIKA ZIARA YAKE WIZARANI


Mheshimiwa Rais, kwa heshima kubwa na taadhima napenda kuchukua nafasi hii kukukaribisha katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Aidha, nachukua nafasi hii kwa niaba ya uongozi na watumishi wote wa Wizara hii kukupongeza wewe binafsi na Chama cha Mapinduzi kwa ushindi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Sisi kama sehemu ya wananchi wa Tanzania tuna imani kubwa na uongozi wako uliojaa hekima, upendo na mwelekeo thabiti wa kuwakomboa Watanzania kiuchumi na kijamii.


Mheshimiwa Rais, naomba kuchukua nafasi hii pia kukushukuru kwa kutuamini; mimi, Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu na Katibu Mkuu Bibi Kijakazi Rajabu Mtengwa na kutukabidhi dhamana ya kusimamia Wizara hii nyeti inayogusa jamii moja kwa moja. Tunakushukuru sana na tunakuahidi kuwa tutatekeleza majukumu uliyotukabidhi kwa uwezo na jitihada zetu zote kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujalia.


Mheshimiwa Rais, wakati wa ziara kama hii mwaka 2006 ulielekeza Wizara kutoa mapendekezo ya jinsi ilivyohitaji kuwezeshwa ili iweze kutimiza majukumu yake yaliyokusudiwa. Nakushukuru na nafurahi kusema kuwa kupitia Baraza la Mawaziri, mwaka 2007 ulikubali Mapendekezo ya Kuimarisha Sekta ya Maendeleo ya Jamii yaliyohusisha ongezeko la bajeti, watumishi na uimarishaji wa taasisi za kuwapatia wananchi maarifa na stadi ili kuwajengea uwezo. Taasisi hizo ni pamoja na Majumba ya Maendeleo na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na kuagiza utekelezaji wake.


2.0 UTEKELEZAJI WA MAELEKEZO YAKO YA MWAKA 2006 NA ILANI YA UCHAGUZI YA CCM YA MWAKA 2005


Mheshimiwa Rais, katika sehemu hii nitatoa muhtasari wa utekelezaji wa maelekezo uliyoyatoa mwaka 2006 ulipotembelea Wizara hii na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005.


Mheshimiwa Rais, katika utekelezaji wa maelekezo yako, bajeti ya Wizara iliendelea kuongezeka ingawa kwa kasi ndogo kutokana na ufinyu wa bajeti ya Serikali ikilinganishwa na majukumu mengi yaliyopo. Aidha, Serikali imekuwa ikitenga fedha kuwezesha Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri kutekeleza majukumu yake. Halikadhalika idadi ya Vyuo vya Maendeleo la Jamii imeongezeka kutoka vinne (4) mwaka 2007 hadi tisa (9) hivi sasa vikitoa mafunzo katika ngazi za Cheti, Stashahada na Shahada. Vyuo hivi vikiendelea kuimarishwa vina uwezo wa kutoa Wataalam wa fani ya Maendeleo ya Jamii wa kutosheleza mahitaji ya kila Kata katika kipindi cha miaka miwili (2) tu. Vilevile, mwaka 2008 Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza Halmashauri kuwaajiri, kuwapatia vitendea kazi na kuwaendeleza wataalam hao. Hata hivyo bado halmashauri hazijaajiri wataalam wa maendeleo ya jamii wa kutosha.


Mheshimiwa Rais, kutokana na sababu hiyo na kwa kuzingatia umuhimu wa wataalam wa maendeleo ya jamii katika kuhamasisha jamii kujiletea maendeleo yake yenyewe, Wizara inaomba ipewe kibali maalum cha kuzipelekea halmashauri wataalam wanaohitimu katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii ili wawapangie kazi katika Kata. Wizara inayo Tange ya wataalam wa maendeleo ya jamii nchini na takwimu zinazoonesha upungufu wa watumishi 1295 katika ngazi ya Kata.


Mheshimiwa Rais, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vimeendelea kufanyiwa ukarabati kadri Wizara ilivyotengewa fedha. Vyuo hivi sasa vimekuwa na mvuto mkubwa kwa wananchi na hivyo kuongezeka kwa idadi ya wanachuo kutoka 24,000 mwaka 2005 hadi 31,000 mwaka 2010. Mafunzo katika vyuo hivi hutolewa ndani na nje ya vyuo. Aidha, vyuo hivi vimeendelea kupatiwa watumishi ingawa wengi wanaopelekwa huko hukimbia baada ya muda mfupi kwa sababu mbalimbali kama vile: umbali na huduma za msingi. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Wizara ilikuwa ikitoa kipaumbele katika kutoa ajira kwa watu ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kujitolea katika vyuo hivyo. Mara nyingi watu hao ni wenyeji wa maeneo hayo hivyo hubakia katika maeneo hayo bila usumbufu mkubwa.


Mheshimiwa Rais, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2005 ilielekeza kuanzishwa kwa Chuo kimoja cha Mafunzo ya ufundi Stadi katika kila Wilaya. Hata hivyo Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii ilihoji uhalali wa kujenga Vyuo vipya wakati viko Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo havitumiki kikamilifu kutokana na uchakavu na kutokupatiwa fedha za kutosha za uendeshaji. Kwa kuzingatia hayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alielekeza utazamwe uwezekano wa kuvitumia Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi kwa madhumuni ya kutolea mafunzo ya ufundi stadi.


Katika hatua za utekelezaji Katibu Mkuu Kiongozi aliunda Kikosi Kazi ambacho kimefanya upembuzi wa kina na kubaini kuwa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vinao uwezo wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na kazi zake za sasa. Aidha, upembuzi huo umebaini kuwa mafunzo ya stadi yanayotolewa sasa hayana budi kuendelezwa kwa kuwa yanatoa fursa ya pekee ya kuwapatia stadi za kazi wahitimu wa elimu ya msingi wapatao 550,000 kila mwaka, ambao hukosa fursa ya kuendelea na elimu ya Sekondari. Hata hivyo taarifa ya upembuzi huo inaonesha kuwa zitahitajika rasilimali zaidi ili kujenga karakana kufanya ukarabati wa majengo na miundombinu na uendeshaji wa shughuli za vyuo hivi.


Mheshimiwa Rais, matokeo ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 yametufundisha kuwa vijana ambao hawana ajira wanaweza kuwa tishio kwa hali ya utulivu na amani iliyopo nchini. Hivyo, Wizara inaamini kuwa ni muhimu sana kuongeza kasi ya kuwapatia vijana maarifa na stadi za kazi ili waweze kujiajiri au kuajiriwa.


Mheshimiwa Rais, kama ulivyosema mwaka 2006 nasi pia tunakiri kuwa wewe ni mdau mkubwa katika maendeleo ya wanawake. Ulitoa wito kwa wanawake kujizatiti katika shughuli zao. Licha ya kuwepo kwa Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na kuanzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira, maarufu kama Mabilioni ya JK, katika miaka mitano ya awali ya uongozi wako tumeshuhudia ndoto ya muda mrefu ya kuanzisha Benki ya Wanawake nchini ikitimia. Hadi kufikia tarehe 28 Februari 2011 mtaji wa benki hiyo ulikuwa shilingi bilioni 4.8. Benki hii imekuwa ikitoa mikopo kwa ajili ya mitaji ya kuendesha biashara pamoja na mahitaji ya binafsi kwa wateja wake mbalimbali. Benki imeshatoa mikopo kwa wanawake na wanaume yenye thamani ya shilingi billioni 8.4 ambapo wanawake ni 3,862 sawa na asilimia 81 na wanaume 855 sawa na asilimia 18. Benki hii tofauti na benki zingine hutoa mafunzo kwa wateja wake na imeshatoa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali wapatao 5,668.


Mheshimiwa Rais, Tunakushukuru sana kwa maelekezo yako uliyoyatoa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mwaka 2010 ya kuitengea Benki hiyo shilingi bilioni 2 kila mwaka kwa muda wa miaka mitano katika kuboresha mtaji wa Benki.


Mheshimiwa Rais, tunakushukuru na kupongeza sana juhudi zako za kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za uongozi wa kisiasa na kiutendaji. Umetekeleza haya kwa kuwateua wanawake katika ngazi mbalimbali.


Mheshimiwa Rais, moja ya changamoto kubwa ambayo imekuwa ikikabili jamii ya Watanzania ni ukatili dhidi ya wanawake, watoto na Albino. Serikali imekuwa ikifanya juhudi kubwa ya kutokomeza ukatili huu ambao umejikita zaidi katika mila na desturi za jamii. Katika kufanikisha azma hii, Wizara imetekeleza mambo mbalimbali ikiwemo:-


(i) Kuendeleza kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia uliyoizindua mwezi Mei 2008 kwa kuelimisha jamii kupiga vita ukatili dhidi ya Wanawake, Watoto na mauaji ya Albino, kwa kutumia filamu maalum iliyoandaliwa na Wizara pamoja na ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2009;


(ii) Kuratibu utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji (2001-2015) hapa nchini, unaotekelezwa na wadau mbalimbali;


(iii) Kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa sheria 274 wakiwemo Polisi, Askari wa Magereza, Mahakimu na Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji.


Mheshimiwa Rais, Wizara yangu imetoa Toleo la Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Mtoto (2008) inayoelekeza watoto kulelewa katika familia na jamii na kuwarejesha wale wanaoishi mitaani katika familia zao. Sera hii inaelekeza upatikanaji wa haki za msingi za watoto.


Mheshimiwa Rais, Wizara inaratibu uenezaji wa uelewa kwa jamii wa Sheria ya Mtoto (2009) yenye lengo la kulinda haki za watoto ikiwa pamoja na haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushirikishwa na Kutobaguliwa. Sheria hiyo inatoa mamlaka kwa Serikali za Mitaa kuwawajibisha wazazi/walezi wanaotelekeza au kutowahudumia kabisa watoto.


Mheshimiwa Rais, Wizara imekamilisha rasimu ya Mkakati wa Jamii wa Kudhibiti Tatizo la Watoto Wanaoishi Mitaani (2009). Mkakati huu unaainisha wajibu wa kila mdau wa maendeleo ya watoto. Aidha, Wizara imeitisha kikao cha Wadau wa masuala ya watoto wakiwemo baadhi ya Wakurugenzi na Mameya wa Majiji, Halmashauri, Waheshimiwa Wabunge na Asasi zisizo za Kiserikali ili kuona jinsi ya kudhibiti tatizo la Watoto wa Mitaani. Kikao hicho kitafanyika tarehe 1 April, 2011 Dar es Salaam.


Mheshimiwa Rais, tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi linachangiwa kwa kiwango kikubwa na wazazi/walezi, jamii na wadau mbalimbali kusahau wajibu wao katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto. Wizara imeandaa rasimu ya Sera Jumui ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambayo ni dira ya utoaji huduma inayolenga kumwezesha mtoto kukua na kufikia utimilifu wake katika nyanja zote za kimwili, kiakili, kimaadili na kimaono ili aweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za ujenzi wa Taifa kuwa raslimali bora.


Mheshimiwa Rais, Wizara kupitia Bodi ya Taifa ya Uratibu wa NGOs na Baraza la Taifa la NGOs iliandaa na kupitisha Kanuni za Maadili ya NGOs ambazo zilitolewa katika Gazeti la Serikali Na. 363 la tarehe 5 Disemba, 2008. Kanuni hizi zinatekelezwa na Baraza la Taifa la NGOs ili kuwezesha NGOs kujidhibiti na hasa zile ambazo hazitekelezi majukumu yao kikamilifu. Baraza tayari limetafsiri Kanuni hizi kwa lugha ya Kiswahili na kuzisambaza kwa mitandao yote ya NGOs katika mikoa na wilaya ili ziingizwe kwenye mipango yao ya kazi. Hata hivyo, Baraza halijafanikiwa kutoa elimu ya Kanuni hizi kwa wadau kutokana na ufinyu wa raslimali fedha.


3.0 CHANGAMOTO


Mheshimiwa Rais, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara inakabiliwa na changamoto zifuatazo:-


(i) Upungufu mkubwa wa rasilimali fedha katika kukidhi utekelezaji wa majukumu ya Wizara kama vile uendeshaji wa vyuo 64 vya Maendeleo ya Jamii na Maendeleo ya Wananchi, utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa na Kikanda inayohusu Usawa wa Kijinsia na Haki za Watoto.


(ii) Upungufu wa Wataalam hususan Wataalam wa Maendeleo ya Jamii katika ngazi ya Kata kwa kiasi cha Watumishi 1,295.


(iii) Kuwepo kwa Mila na Desturi zinazoleta madhara kwa wanawake na watoto.


(iv) Matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


(v) Ongezeko kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.


4.0 MAENEO YA KIPAUMBELE KWA MWAKA 2010-2015


Mheshimiwa Rais, pamoja na ukweli kuwa Wizara yangu ni mtambuka na hivyo kuchangia kwa namna tofauti katika utekelezaji wa vipaumbele vya kitaifa, Wizara hii itatoa mchango mkubwa zaidi katika utekelezaji wa Kilimo Kwanza na kuongeza ajira kupitia vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Aidha, Wizara itaendelea kuimarisha upatikanaji wa mitaji kwa wanawake ili waweze kukabiliana na umaskini wa kipato.


Vipaumbele mahususi vya Wizara ni kama ifuatavyo:


(i) Kusimamia na kuimarisha utoaji wa mafunzo ya taaluma ya Maendeleo ya Jamii katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na mafunzo ya maarifa, ujuzi na stadi katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi;


(ii) Kuwajengea uwezo wanawake na wanaume ili washiriki katika ngazi zote za utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya maendeleo na kufaidika sawa katika maendeleo hayo;


(iii) Kuratibu utekelezaji wa Mikataba ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa inayohusu ustawi, haki na maendeleo ya wanawake na watoto;


(iv) Kuimarisha usajili, uratibu na ufuatiliaji wa shughuli za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika ngazi mbalimbali.


(v) Kuwapatia Wanawake mafunzo kwa lengo la kuwawezesha kuunda vikundi vya kuweka na kukopa sambamba na Ushirika wa kuweka na kukopa ili waweze kukopesheka kwa urahisi na Benki na Asasi husika.




No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.