MKURUGENZI wa shindano la Taifa la Miss Utalii, Gideon Chipungahelo, amedaiwa kumtwanga fundi mitambo aliyekuwa akisimamia suala la taa katika ukumbi wa Hoteli lilipofanyika shindano hilo hivi karibuni mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Chipungahelo, alimfuata na kuanza kumporomoshea magumi mazito fundi mitambo huyo baada ya umeme kuzimika ghafla ukumbini humo wakati shindano hilo likiendelea huku likiwa linarushwa live na moja ya Kituo cha Televisheni.
Baada ya kutokea tukio hilo, Chipungahelo aliyekuwa Mc wa shindano hilo huku 'akihozi' kuongoza kila idara iliyokuwa ikishughulika na shindano hilo, alishuka jukwaani huku likiwa limetawala giza totoro na kutimua mbio kuelekea katika chumba alichokuwapo jamaa huyo.
Ghafla mashabiki wa shindano hilo waliokuwa ukumbini humo pamoja na mapaparazi, walimsikia jamaa huyo akipiga kelele za kuomba msaada kwa kupokea kipigo kitakatifu kutoka kwa Chipungahelo, aliyekuwa akifanya hivyo huku akiwaka kwa sauti, “Unataka kuniharibia shughuli”. Alisikika akisema Chipungahelo.
Hata hivyo mashabiki wa shindano hilo walisikika wakilalama ukumbini humo kutokana na utaratibu wa Mkurugenzi huyo anavyoendesha shindano hilo, na kumtupia lawama lukuki kwa kupanga matokeo na kumpa ushindi mshiriki ambaye wao wanazani hakustahili kushinda.
Baadhi ya wazazi wa washiriki hao walisikika wakilalama ukumbini humo kuwa hawakubaliani na matokeo hayo kwa vile washindi wa tatu bora waliochaguliwa hawakukidhi vigezo na hawakua na mvuto mbele ya mashabiki ukumbini humo.
Shindano hilo liliwaboa watu zaidi pale lilipovunja rekodi ya kuchelewa kuanza, ambapo lilianza mida ya saa tano usiku na kumalizika saa kumi na mbili kasoro za alfajiri siku iliyofuata.
Akizungumza na Sufianimafoto Mkurugenzi wa Shindano hilo, Gideon Chipungahelo, alikili kutokea kwa mshike mshike huo na kusema kuwa, alilazimika kumtwanga magumi fundi huyo baada ya kugundua kuwa alikuwa amehujumiwa kutokana na shindano hilo kuwa likirushwa live.
“Unajua muda mwingine inabidi uwe Baunsa tu kwani niligundua mipango ya wazi kabisa ya kuniujumu na kuharibu shindano langu tangu mapema na ndiyo maana baada tu ya kutokea tukio hilo la kukatika kwa umeme nilimwendea moja kwa moja aliyekuwa akihusika na idara hiyo, ambaye hakuwa na majibu ya kuniridhisha,
Na ndiyo hasa sababu iliyonifanya kuanza kumtwanga magumi potelea mbali kama nilionekana tofauti kwa muda ule kwani tayari nilishapandwa na ghadhabu kutokana na kuharibikiwa tena mbele ya mashabiki waliokuwapo ukumbini na watu waliokuwa katika Luninga zao majumbani wakifuatilia shindano hilo” alisema Chipungahelo.

No comments:
Post a Comment