BENKI ya Exim Tanzania imeongeza faida ya pato lake kufikia sh. bilioni 16.6/- hadi mwishoni mwa mwaka jana ikiwa ni ongezeko la 66.7% ukilinganisha na pato la sh. bilioni 9.99 la mwaka wa fedha 2009.Mafanikio hayo yanaifanya benki hiyo kuwa kinara wa ongezeko la faida katika sekta ya kibenki nchini inayoonyesha kukua kwa kasi katika ufanisi na ubunifu katika utendaji wake.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na benki hiyo jana na kusainiwa na Meneja Mkuu Dinesh Arora, hatua hiyo ya maendeleo ya kasi inatokana na ushirikiano mzuri kiutendaji uliojengekana miongoni mwa wadau wa benki hiyo.
“Tumeongeza pato letu kwa 66.7% na kufika sh. bilioni 16.6 hadi ilipofikia mwishoni mwa mwaka jana kutoka sh. bilioni 9.99 za mwaka 2009, hivyo ni hatua ya kupongezwa”, ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza faida ya uendeshaji wa benki kwa mwaka wa fedha 2010 imeongezeka kwa asilimia 60% na kufikia shilingi 23.22 bilioni dhidi ya shilingi bilioni 13.87 ukitoa pato la ziada la shilingi bilioni 4 lililopatikana mwisho mwa mwaka 2009.
Inafafanua kuwa pato la benki kwa ujumla limeongezeka kutoka sh.bilioni 127 na kufikia sh. bilioni 710 ilipofika mwishoni mwa Desemba 2010 na kuifanya Benki ya Exim kuwa miongoni mwa benki 6 kubwa nchini kuwa na rekodi nzuri katika pato la jumla.Katika gawio la ‘gross NPA ratio’ benki ya exim imeshuka kufikia 4.1% ilipofika Desemba 2010 kutoka 4.3% ya Desemba 2009.
Katika kuendelea mbele, Benki ya Exim imeweka kipaumbele kwenye uongozi wa NPA na kufanya tathimini ya kila mara katika kuhakikisha kitengo hicho kinapanda kiubora.
“Tumeonekana kushuka kidogo katika sehemu ya NPA lakini benki inafanya jitihada za makusudi kuhakikisha kuwa mikakati mipya ya kusaidia kuinuka kwa kitengo hicho inawekwa”, inasisitiza sehemu ya taarifa hiyo.
Benki ya Exim Tanzania ina matawi 22 katika sehemu mbalimbali za nchi ikiwa ni pamoja na kuwa na uendeshaji wa kibenki katika Visiwa vya Comoro zinazoongozwa na huduma ya ATM ambapo Tanzania zipo 45 na 25 nje ya Tanzania. Katika kuhakikisha benki hiyo inaongeza ufanisi wake kiutendaji, mwaka jana imeajiri wafanyakazi wengine 150 wakiwemo wataalamu watatu kutoka nje ya nchi ikiwa ni kuendelea kuonyesha mfano kwa kuwavutia watanzania waishio nje, kurudi nyumbani na kufanyakazi.
No comments:
Post a Comment