Na Sufianimafoto Reporter, jijini Mshiriki wa shindano la kunengua nyimbo za bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, linalojulikana kama ‘Kimwana Manywele wa Twanga Pepeta’, Edna Amani ‘Dinna Delicious’, ametamba kuwagalagaza washiriki wenzake msimu huu.
Akizungumza na mtandao wa Sufianimafoto Dar es Salaam leo mchana, Dinna alisema kuwa matumaini yake hayo yanatokana na jinsi anavyojiamini katika kuondoka vilivyo staili za bendi hiyo, akiamini hakuna atakayemshinda katika unenguaji wa nyimbo za bendi hiyo. Alisema kuwa mbali na kujiamini, pia umahiri wake wa kunengua nyimbo mbalimbali, anadhani hakuna anayeweza kumfikia miongoni mwa washirki wenzake wa shindano hilo kwa jinsi alivyokwishakuwa nao kwa kipindi kifupi.
“Mimi ninatisha katika uchezaji, sidhani kama kuna atakayeniweza, wote watakaoshiriki, watakuwa ni wasindikizaji tu, lazima nitwae taji hilo,” alijigamba mrembo huyo.
Hata hivyo, aliwataka washiriki wengine wasije kujitoa kwa kumhofia yeye, kwani ushiriki wao tu hata kama hawatatwaa taji, itakuwa ni changamoto tosha kwao.
Alisema kuwa tayari ameshajipanga vilivyo aweze kuonyesha cheche zake, pindi washirki watakapoanza kuchuana rasmi Mei 6 mwaka huu ndani ya Ukumbi wa Sun Cirro, jijini, ambapo tayari ameshaanza mazoezi binafsi mbali na ya pamoja na wenzake chini ya mwalimu wake ambaye hakutaka kumtaja jina kwa kuhofia fitina za mjini.
Kwa upande wake, mratibu wa shindano hilo, Maimartha Jesse, amesema kuwa mshindi atakayepatikana kwa mwaka huu, atazawadiwa Duka la Vipodozi lenye thamani isiyopungua Sh milioni tano.
Alisema kuwa dula hilo litakuwa katika wilaya ya Kinondoni ambapo litalipiwa kodi na leseni ya mwaka mzima. Washiriki wanatarajiwa kuingia kambini kuanzia kesho kwa ajili ya mazoezi, ambayo watajifua chini ya kiongozi wa wanenguaji wa Twanga Pepeta, Kassim Mohamed 'Super K'.
No comments:
Post a Comment