Bondia Japhet Kaseba (kushoto) akichuana na Mada maugo wakati wa pambano lao lisilo la ubingwa la raundi nane lililofanyika kwenye Ukumbi wa PTA Sabasaba Temeke Dar es Salaam jana. Pambano hilo lilimalizika katika raundi ya saba baada ya mabondia hao kuchezeana faulo bila mwamuzi kusimamisha mchezo na Kaseba kuamua kuvua glovz kugoma kuendelea na pambano na Maugo kutangazwa mshindi.
******************************************************************
Na Sufianimafoto Reporter,jijini
BONDIA Japhet Kaseba jana alikubali yaishe na kuamua kuvua glovz zake kabla ya pambano lake na Maugo kumalizika katika raundi ya saba ya mchezo na kufanya mpinzani wake Mada maugo kuibuka na ushindi katika pambano hilo la raundi nane lisilo la ubingwa.
Kabla ya kuanza kwa pambano hilo rais wa TPBO Yassin Abdallah ‘Ustaadh’, alipanda jukwaani na kutangaza utaratibu utakaotumika kuchezesha pambano hilo na jinsi ya kutoa point, ambapo alisema kuwa pambano hilo litachezeshwa na mwamuzi mmoja atakayefanya kazi zote za kuchezesha na kutoa pointi.
Alisema kuwa kutokana na uzoefu wa mapambano kama hayo yaliyopita kumekuwa na malalamiko mengi kuhusu mabondia kuonekana wamependelewa na baadhi ya waamuzi na hivyo ili kuepuka malalamiko kama hayo wameamua kutumia mtindo huo ambao hutumika hata kimataifa.
“Hatutaki baada ya pambano hili kuona mashabiki wakilalamika kuwa mchezaji wao ameonewa na ndiyo maana tumeamua kutumia utaratibu huu ambao umekuwa ukitumiwa na katika nchi nyingi zilizoendelea ili kusitokee malalamiko” alisema Ustaadh.
Wakati pambano hilo likiendelea Kasema aliweza kumpeleka chini mara mbili mpinzani wake katika raundi ya tatu na ya nne, raundi ya tano na sita Maugo aliweza kucharuka na kubadili mchezo kwa kumshambulia zaidi kaseba, lakini katika raundi ya saba Maugo alicheza faulo kwa kumsukuma mpinzania wake kwa goti bila mwamuzi kuona na kumfanya Kaseba kugusa chini kwa mikono.
Baada tu ya kuinuka Maugo aliendela kumshambulia mpinzani wake huku Kaseba akiinua mkono kumuonyesha mwamuzi kuwa Glovz yake ilikuwa imefunguka bila kujali maugo aliendelea na mashambulizi yaani ‘kuskoo’ na mwamuzi kushindwa kusimamisha pambano jambo ambalo lilimuudhi Kaseba na kuamua kucheza mchezo aliouzoea.
Kaseba alitumia mguu kumwangusha mpinzani wake Maugo aliyekwenda chini kama gunia na kufanya pambano hilo kusimama, na kuzuka vurugu zilizowafanya mashabiki wa pande zote mbili kupanda jukwaani huku wao kwa wao wakishambuliana na kuamuliwa na askari.
Wakati huo tayari Kaseba alishaamua kususa na kuvua glovz zake, pamoja na kushawishiwa na watu wake Mashabiki na kocha wake kuvaa glovz ili kuendelea na pambano lakini alikataa katakata huku akitaka kutoka nje ya ulingo na kurudishwa na mashabiki wake hadi hapo mwamuzi alipoamua kushika Mic na kutangaza mshindi.
“Katika pambano hili kufuatana na sheria za ngumi kote Duniani tayari mshindi ameshajulikana kutokana na mmoja kuwa tayari ameshaamua kuvua glovz nah ii inaashiria kuwa hawezi kuendelea na mchezo, hivyo katika pambano hili siku ya leo mshindi ni Mada Maugo katika raundi ya saba” alisema mwamuzi huyo huku akiwa tayari ameshazungukwa na askari.
Baada tu ya kutangaza matokeo hayo mashabiki walianza kurusha viti ulingoni huku wa upande wa pili wakimbeba Maugo huku wakiimba na kuondoka zao.
Mashabiki wa Mada Maugo wakimbeba juu juu Mada huku wakishangilia ushindi, baada ya kumalizika kwa pambano hilo na kutangazwa mshindi. Bondia Yohana Robert (kulia) akimchakaza mpinzani wake Said Zungu, wakati wa pambano lao la utangulizi la raundi 10 la kuwania ubingwa wa TPBO, ambapo Yohana alishinda pambano hilo katika raundi ya nne baada ya Zungu kutokwa na damu nyingi usoni jambo lililomfanya kutoendelea na pambano hilo Yohana kutwaa mkanda.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, David Misime, akimvisha mkanda Yohana Robert baada ya kuibuka mshindi katika pambano lake la kuwania ubingwa wa TPBO na mpinzani wake, Said Zungu.
Mohamed Matumla (kulia) akichuana na mpinzani wake, Sadiq Momba, bondia mwenye makeke awapo jukwaani kama anavyoonekana akikwepa konde kwa staili ya aina yake huku mguu mmoja akiwa ametinga kiati na mguu mmoja Soksi, hii ilitokea wakati alipokuwa akijaribu kubadilisha viatu kutokana kuteleza mara kadhaa, kwa bahati mbaya muda wa mapumziko ukamalizika na kumlazimu kurejea ulingoni bila kiatu kimoja.
Bondia Rashid Matumla akimpa mdogo wake Mohamed Matumla, mbinu za kumkabili mpinzani wake, Sadiki Momba baada ya kuona mdogo wake akizidiwa kimchezo. Hata hivyo Matumla alishinda pambano hilo kwa pointi.
No comments:
Post a Comment