Habari za Punde

*MADEREVA WA MALORI WAFUNGA MAGETI YA MILLENNIUM BUSINESS PARK KUPINGA USHULU WA SH 15,000 ZA MAEGESHO

WAFANYABIASHARA waliopanga katika jengo la Millennium Business Park lililopo Barabara ya Shekilango jijini Dar es Salaam, wameulalamikia uongozi na wamiliki wa majengo hayo ya biashara kwa kuwataka wapangaji kulipia maegesho ya kila gari linaloingia kushusha mzigo kiasi cha Sh 15, 000 kila moja, jambo ambalo limepingwa na madereva wa magari hayo walioamua kuweka mgomo na kufunga mageti yote ya kuingia na kutoka katika eneo hilo. Madereva hao wamefikia hatua hiyo baada ya kufika katika geti la kuingia katika maghala hayo kwa lengo la kushusha mizigo inayotoka Bandarini na kuzuiliwa na uongozi wakitakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha tangu juzi jioni na kuwalazimu madereva hao kukesha kwenye magari yao yaliyokuwa tayari yameshaunda foleni kubwa huku wakilinda mizigo hiyo. Kutokana na hatua hiyo madereva walipitisha uamuzi wa kuzuia mageti yote ya kuingia na kutokea kwa kuweka magari yao katika mageti hayo ili kuwazuia wapangaji na wateja wanaohitaji kuingia kupata huduma ambao wengi hufika nyakati za asubuhi. Baadhi ya wafanyabiashara wenye frem katika jengo hilo walipofika asubuhi walishindwa kuingiza magari yao kutokana na mageti yote kuzuiwa na magari hayo makubwa yenye makontena na mizigo huku madereva hao pia wakitaka kulipwa ujira wa kukesha wakilinda mizigo hiyo ambavyo haikuwa kazi yao jambo ambalo lilizua utata mkbwa na kumfanya Meneja wa magodauni hayo kukimbia na kujifungia ndani na madereva nao kutokomea kusikojulikana na kusababisha msongamano mkubwa wa magari mahala hapo. Baadhi ya wafanyabiashara hao walionekana wakitaka kujua hatma yao ya kuendelea kuchelewa kufanya biashara na kukosa wateja wao toka asubuhi, lakini juhudi za kuonana na Meneja ziligonga ukuta baada ya meneja huyo kujifungia ndani na kutotaka kuonana na yeyote kwa muda huo. “Kuanzia muda huu hasara yeyote nitakayoipata nawaletea ninyi Invoice mnilipe, siwezi kukubari kupata hasara kwa sababu ya ninyi kukosana na kushindwa kuelewana na wapangaji wenu, hawezi mtu mmoja tu ndiyo atuendeshe watu wote katika jingo hili kwa kuzuia mageti wengine tusiendelee na biashara zetu” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao aliyefika ofisini kwa Meneja. Aidha Karani wa Meneja huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake, alitoa majibu kuwa Meneja hawezi kuonana na watu kwa muda huo kwani alikuwa na shughuli kubwa na kumsemea kuwa Uongozi ulitoa barua ya kuhusu wateja wao kulipia gharama ya Sh 15,000 kwa kila gari ambayo ilikabidhiwa kwa wafanyabiashara hao tangi tarehe 1 mwezi huu. “We uliona wapi mwenyenyumba anakupangisha chumba kisha akiona unagari basi aongeze mashariti eti inabidi ulipie na gari lako kwa sababu linapaki kwenye Uwanja wangu, yaani mpangaji ulipie kodi ya nyumba na egesho la gari?, hii sijawahi kuona duniani kote” alisema mmoja wa wafanyabiashara hao. Pia Msemaji wa Kampuni ya Sunda Tanzania Ivestment iliyomo katika majengo hayo, imetoa malalamiko yake kuwa imepata hasara isiyopungua Sh. Milioni 5 kutokana na godauni lao kuvuja nyakazi hizi za mvua na kufikisha kwa uongozi bila kupatiwa ufumbuzi wa kufanyiwa marekebisho hadi kufikia kuharibika kwa mali zao zenye gharama hizo.

Baadhi ya wafanyabiashara walio na ofisi ndani ya majengo hayo wakiwa nje, baada ya kushindwa kupitisha magari yao kuingia ndani. Wahindi wanaodaiwa kuanzisha utaratibu huo wakisimamia magari katika geti la pili baada ya kufunguliwa huku wakiwakomand walinzi kuruhusu magari bila kuandikishwa getini hapo kinyume cha utaratibu.
Wahindi hao wakilinda mlango wa Meneja aliyekuwa amejifungia ndani ambapo hatutaka kuonana na mtu.
Baadhi ya wafanyabiashara hao wakijadiliana nje ya ofisi hizo kutafuta ufumbuzi wa kupitisha magari yao.
Baadhi yao walianza kuhamisha vitendea kazi vyao katika ofisi hizo ili kuendelea na kazi zao katika mahala pengine walikotafuta kwa muda.
Hili ndilo geti la pili la kutokea ambalo pia lilikuwa limefungwa na malori hayo, kama unavyoona gari hilo lilivyokaa getini hapo kwa kukatiza njia ili gari jingine lisiweze kupita.
Wapakuaji mizigo wakiwa nje ya magodauni hayo wakisubiri kukamilika kwa utaratibu ili magari yaingie waanze kazi ya kushusha mizigo.
Huku ni uapnde wa pili wa geti la kutokea pia kukiwa na foleni kutokana na Lori hilo kuziba njia. Madereva wa malori hayo waliegesha magari hayo toka juzi jioni walipofika kwa ajili ya kupakua mizigo na kukuta utaratibu huo uliowekwa na wamiliki kinyume na mkataba wa wapangaji.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.