TANZANIA NI NCHI SALAMA WAWEKEZAJI JITOKEZENI KUWEKEZA, ASEMA BALOZI MAAJAR
Anna Nkinda – Phoenix, Arizona
Wawekezaji, watalii pamoja na wataalamu mbalimbali wametakiwa kutoogopa kuja kufanya kazi nchini kwa kuhofia usama wao, kwani Tanzania ni nchi yenye amani, usalama na upendo.
Wito huo umetolewa jana na balozi wa Tanzani nchini Marekani Mwanaidi Sinare Maajar wakati akijibu swali la mwanafunzi wa chuo kikuu cha Thunder School of Global Management kilichopo mjini Phoenix nchini Marekani Anishe Patel ambaye alisema kwamba amekuwa akisikia katika vyombo vya habari kuwa Tanzania inakabiliwa na tatizo la usalama.
Balozi Majaar alisema kuwa vyombo vingi vya habari vya nchi za nje vimekuwa vikiripoti taarifa ambazo si sahihi kuhusu Tanzania na hivyo kupotosha ukweli wa mambo ukweli uliopo ni kuwa kutokana na ripoti za Shirika la Kimataifa la Upelelezi la Nchini Marekani (F.B.I) Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuwa na usalama wa kutosha pia haipo katika orodha ya nchi zenye kuwa na matukio ya uhalifu.
“Nchi yetu ni ya amani tumekuwa tukisikia huku Marekani pamoja na nchi zingine mara kwa mara kuna matatizo makubwa ya matukio ya ujambazi wa kutumia silaha jambo ambalo ni nadra kutokea nchini Tanzania tunawakaribisha mje kuwekeza, kufanya biashara na kutalii nchini Tanzania”, alisema Balozi Majaar.
Aliendelea kusema kuwa watu wako huru kutembea katika mitaa mbalimbali bila ya kukutana na tatizo la uhalifu na kutoa mfano wa jiji la Dar es Salaam ambalo ni kubwa kuliko majiji yote nchini Tanzania na liko salama jambo ambalo ni nadra kutokea katika miji mingine mikubwa hapa Duniani ambayo haina usalama.
Aidha kuhusiana na suala la miundombinu balozi huyo alisema kuwa hivi sasa kuna miradi mbalimbali ya ujenzi wa barabara inayoendelea ambayo ni matokeo ya makubaliano baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Marekani chini ya MCC challenge account na ifikapo mwaka 2013 tatizo la barabara litakuwa limemalizika nchini Tanzania.
Kuhusina na suala la utalii Balozi Majaar alisema kuwa Tanzania imejaliwa kuwa na vivutio vya aina mbalimbali ukiwemo mlima Kilimanjaro, visiwa vya Zanzibar na mbuga za wanyama za Ngorongoro, Mikumi na Serengeti ambako kuna wakati wanyama wanahama kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.
Balozi huyo alisema, “Ninawakaribisha sana nchini Tanzania mje kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo ninauhakika kufika kwenu kutawapa picha halisi ya jinsi Tanzania ilivyo na si kama ilivyo sasa mnapata taarifa sahihi na zingine si sahihi kutoka katika vyombo vya habari”.
Anishe Patel alitaka kujua hatua ambazo Serikali imezichukua ili kukabiliana na tatizo la uhalifu kwani kutokana na taarifa zinazoripotiwa na vyombo vya habari ni kuwa suala la uhalifu Tanzania ni kubwa kwa asilimia 34 kwa mwaka hii inamaana kwamba Polisi wameshindwa kufanya kazi yao ipasavyo.
Patel aliuliza, “Nimesikia kuwa moja ya hatua iliyochukuliwa na Serikali ni kuanzishwa kwa vikosi vya sungusungu je kuna mpango gani wa kuhakikisha kuwa kuna usalama wa kutosha katika miji iliyopo nchini Tanzania ikiwa ni pamoja na Dar es Salaam?”.
Balozi Maajar aliongozana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete chuoni hapo kwa ajili ya kuwasilisha mada kuhusu Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) jinsi inavyofanya kazi ya kumuinua mwanamke wa kitanzania, kuhakikisha watoto wa kike wanapata nafasi ya kusoma na kuepuka mimba za utotoni na kuhakikisha kuwa vifo vya watoto wachanga na kina mama wajawazito vinapungua.Mwenyekiti wa WAMA Mama Salma Kikwete (kulia) ,Rais wa Thunderbird School of Global Management Rais Daktari Angel Cabrera, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Mwanaidi Maajar, Rais wa Project C.U.R.E Daktari Douglas Jackson pamoja na mjumbe wa Bodi ya WAMA Zakhia Meghji, wakimsikiliza kwa makini mwanafunzi wa Kitanzania anayesona chuoni hapo, Niky Choksi( hayupo pichani) akitoa maelezo yake ya masomo ya kozi anayosomea chuoni hapo. Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (mbele kushoto) pamoja na ujumbe wake wakiongozwa na Rais wa Thunderbird School of Global Management Daktari Angel Cabrera (suti) kuangalia sehemu za maeneo ya shule. Mama Kikwete pia ameweza kufanya mazungumzo na wanafunzi wa chuo hicho. Picha Zote na Mwanakombo Jumaa-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment