Habari za Punde

*MAMA SALMA KIKWETE AHIMIZA MCHEZO WA BAO UPELEKWE MASHULENI

Na Mwanakombo Jumaa-MAELEZO

Mlezi wa Shirikisho la Mchezo wa Bao Tanzania (SHIMBATA) Mama Salma Kikwete, ameshauri mchezo wa jadi wa bao upelekwe mashuleni ili kuwajengea uwezo zaidi wanafunzi kufikiri katika masomo yao .


Mama Salma Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA amesema hayo leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, wakati wa hafla fupi iliyofanyika maalumu kwa ajili ya kumkabidhi bao la mchezo wa jadi na Rais wa Shirikisho la mchezo wa bao nchini, Monday Likwepa.


Wakati wa makabidhiano hayo Mlezi huyo wa SHIMBATA amesema mchezo wa bao huwasaidia wanafunzi wengi kuelewa somo la hesabati kwani hutumia akili zaidi wanapocheza mchezo huo.


“Nilipokuwa mdogo nilicheza michezo ya jadi mingi ukiwemo mchezo wa bao, lakini nasikitika kuona michezo mingi ya jadi haichezwi tena na watoto wa siku hizi na kuwa katika hatari ya kutoweka,” alisema.


“Baadhi ya watu wanadhani kuwa mchezo wa bao ni mchezo wa watu wavivu, ukweli mchezo wa bao sio mchezo wa watu wavivu bali ni mchezo kama michezo mingine na unafaa kuendelezwa.” alisema Mama Salma


Aidha alisema kuwa kama mchezo wa bao ungekuwa mchezo wa watu wavivu, Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere, asingekuwa mchezaji na mpenzi mkubwa wa mchezo huo.


Rais wa SHIMBATA, Likwepa ameeleza wakati wa hafla hiyo kuwa, lengo la kumkabidhi bao Mama Salma Kikwete ni kumkumbusha Mlezi huyo, Serikali pamoja na jamii kwa ujumla kuwa nchi yetu ina michezo mingi ya jadi ambayo inafaa kupewa kipaumbele na Serikali kama michezo mingine.


Mbali na bao Vilevile Rais Likwepa alikabidhi kitabu cha mchezo wa bao kilichoandikwa kwa lugha ya Kiitaliano pamoja na barua ya mwaliko kutoka Italia kwa SHIMBATA kushiriki shindano la kimataifa hapo baadae.


Mama Salma Kikwete baada ya kupokea kitabu hicho, ameshauri viongozi wa SHIMBATA kutafsiri kitabu hicho katika lugha ya Kiswahili ili watanzania waliowengi waweze kusoma na kuelewa kuhusu mchezo huo.


Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA na mlezi wa shirikisho la mchezo wa jadi wa Bao Mama Salma Kikwete (kushoto) akicheza bao na Rais wa mchezo huo baada ya hafla fupi ya kukabidhiwa bao hilo iliyofanyika jijini Dar eS salaam leo. Picha na Mwankombo Jumaa- MAELEZO

Mama Salma Kikwete (kwenye kilemba) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Shirikisho la mchezo wa bao Tanzania baada ya hafla hiyo.






No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.