Habari za Punde

*OCAMPO AITOLEA JICHO KWA KARIBU LIBYA




Mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu, anafanya uchunguzi wa kutoa amri ya kukamatwa kwa watu watatu kuhusiana na uhalifu dhidi ya ubinaadam nchini Libya


Luis Moreno Ocampo hakutaja majina yoyote, lakini ameliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa uhalifu huo bado unaendelea.


Majeshi ya kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi yamekuwa yakipambana na watu wanaopinga serikali kwa miezi miwili.


Watu 500


Katika taarifa yakle kwa baraza la usalama, Bw Moreno-Ocampo amesema kati ya watu 500 na 700 wanakadiriwa kuuawa nchini Libya, katika mwezi Februari pekee.


Hajataja majina ya anaotaka kutoa amri hiyo ya kukamatwa, ambayo amesema anatarajia kuiwasilisha katika wiki chache zijazo.


Mwandishi wa BBC katika Umoja wa Mataifa Barbara Plett amesema amri hizo zitalenga udhibiti wa awali dhidi ya waandamanaji.


Tuhuma nzito


Ripoti zinadai kuwepo kwa uhalifu ambao unasemekana ulifanywa kwa mujibu wa maagizo yaliyotolewa na watu wachache wa ngazi za juu, na kuongeza tetesi kuwa Kanali Gaddafi na watu wake wa karibu huenda wakashitakiwa.


Ofisi ya mwendesha mashitaka pia inaendelea na uchunguzi kuhusu tuhuma nzito za ubakaji, na taarifa kuwa makundi ya watu wenye hasira katika mji wa Benhgazi waliua Waafrika wengi waliodhaniwa kuwa ni mamluki.


Mwandishi wetu anasema Bw Moreno-Ocampo ameonya kuwa atafungua kesi zaidi kadri zitakavyowezekana.


Meli ya misaada


Wakati huohuo, meli ya misaada imetia nanga katika mji wa Misrata, licha ya mashambulio yanayoendelea kufanywa na majeshi ya wanaomuunga mkono Gaddafi.


Meli hiyo inayoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) imepeleka tani 180 za chakula na dawa mjini Misrata, baada ya kushindwa kutia nanga kwa siku nne kutokana na mapigano karibu bandarini.


Meli hiyo iliondoa wakimbizi 800 wa Kiafrika na kutoka Asia, lakini walikuwa na matumaini ya kuondoa watu wengine 1,000.





No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.