Kusudio la kukata rufaa hiyo limewasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa washitakiwa hao, Majura Magafu.
Wakili Magafu alidai wateja wake hawakuridhika na hukumu hiyo, hivyo amewasilisha kusudio la kukata rufani pamoja na mambo mengine kupitia mwenendo wa kesi hiyo na kisha kuwasilisha rufani kamili katika Mahakama Kuu.
Rufaa hiyo imewasilishwa ikiwa ni siku tatu baada ya washitakiwa hao kuhukumiwa adhabu hiyo ya kifungo cha miaka mitano sanjari na kurejesha fedha hizo la watafilisiwa kwa mujibu wa sheria.
Katika kesi hiyo iliyotolewa hukumu Mei 23, mwaka huu, washitakiwa hao walidaiwa kutenda makosa nane yakiwamo kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha Sh bilioni 1.8, mali ya BOT kwa njia ya udanyifu kwenye akaunti wakijaribu kuonyesha kampuni yao ya Kiloloma and Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai India.
Hata hivyo kampuni hiyo haikuwahi kuwepo wala kusajiliwa na Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela).
Hata hivyo, katika mashitaka hayo, shitaka la kwanza la wizi lilifutwa kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha hivyo kosa hilo.
Katika hukumu hiyo, Mahakama ilisema mshitakiwa wa kwanza katika kosa la pili, atatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela, katika shitaka la tatu washitakiwa wote watatumikia adhabu ya miaka mitano jela.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ilvin Mgeta, alisema kwa shitaka la tano mshitakiwa wa pili pekee atatumikia kifungo cha miaka miwili jela, shitaka la sita wote kwa pamoja watatumikia miaka mitatu jela na katika shitaka la saba na la nane washitakiwa wote watatumikia adhabu ya kifungo cha miaka mitatu jela.
Maranda na Farijala wamekuwa ni washitakiwa wa kwanza wa kesi za EPA zilizofunguliwa mahakamani hapo, kuhukumiwa adhabu hiyo ambapo kesi hiyo ilifunguliwa Novemba 4, mwaka 2008.
No comments:
Post a Comment