Habari za Punde

*KCB TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA MAZINGIRA KWA KUPANDA MITI 21,000

Wafanyakazi wa Benki ya KCB Tanzania wakigawa juisi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Msongola walioshiriki uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti 21,000 kuadhimisha siku ya jamii na mazingira duniani uliofanyika katika Kijiji cha Msongola Chanika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya KCB Tanzania wakimwagilia maji katika moja ya mti waliyopanda wakati wa wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa Benki ya KCB Tanzania Christine Manyenye akiwaongoza wafanyakazi wenzake kupanda miti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti 21,000 kuadhimisha siku ya jamii na ya mazingira duniani iliyofanyika katika Kijiji cha Msongola, Chanika jijini Dar es Salaam.
Diwani wa Kata ya Msongola, Angela Malembeka akipanda mti wakati wa uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti 21,000 kuadhimisha siku ya jamii na mazingira duniani uliofanyika katika Kijiji cha Msongola Chanika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya KCB Tanzania Moezz Mir na katikati ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano wa benki hiyo Christine Manyenye.
*************************************************************************************

BENKI ya KCB Tanzania kwa kushirikiana na uongozi wa kijiji cha Chanika- Msolongola mwishoni mwa wiki waliendesha zoezi la upandaji miti ambapo miti zaidi ya 9000 ilipandwa kijijini hapo.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo , Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Tanzania Dk Edmund Mndolwa, alisema zoezi hilo lilikuwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya jamii ambayo huazimishwa na benki hiyo kila mwaka.

Dk Mndolwa alisema zoezi hilo linalenga kuiunga mkono serikali katika suala la utunzaji wa mazingira na ni muendelezo wa shughuli mbalimbali ambazo benki ya KCB Tanzania inafanya kwa ajili ya jamii mwaka hadi mwaka.

Alisema kuwa kila mwaka mbali na misaada ambayo hutolewa na benki hiyo, benki huchagua sekta moja ambayo huelekeza misaada wakati wa maadhimisho ya wiki ya jamii.

“Mwaka huu siku ya jamii tumeielekeza kwenye sekta ya mazingira. Mwezi Oktoba tutaadhimisha tena wiki ya jamii ambapo tutaangalia na kusaidia sekta ya elimu,” alisema.

Mwenyekiti huyo wa bodi aliongeza “Leo katika kuadhimisha siku ya jamii tutapanda miti 9000 katika shule ya sekondari na shule ya msingi Msongola pamoja na Zahanati ya Msongola. Idadi ya miti tutakayopanda nchi nzima ni 21,000. Miti mingine itapandwa Moshi, Arusha, Mwanza, Morogoro na Zanzibar.

Mweka hazina wa Taasisi ya Imitra Bwana Aloys Mawanga ambao ni wasimamizi wa mradi huo wa upandaji miti alisema ni mara ya pili kwa benki hiyo kushirikiana nao katika mpango huo wa utunzaji mazingira na awamu ya kwanza mpango huo waliutekeleza Kibaha mkoani Pwani.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Msolonga Angelina Malembeko aliishukuru benki ya KCB kwa niaba ya uongozi wa kata na kijiji na kuihakikishia kuwa miti hiyo italindwa na kutunza ili ikue na kuleta faida katika jamii.

“Napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa niaba ya wana Msongola. Huu ni msaada wa maana sana ambao utatusaidia sisi pamoja na watoto wetu, nawahakikishieni kuwa miti hii italindwa na kutunzwa hadi kukua, alieleza

Zoezi hilo la upandaji miti, lilishirikisha wafanyakazi wa benki ya KCB Tanzania wa Dar es Salaam , wanafunzi wa shule ya sekondari na msingi Msongola, viongozi wa kata pamoja na wanakijiji.


No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.