Baadhi ya waumini wa kanisa hilo wakiwa na Mbuzi waliowatoa kwa ajili ya Harambee ya kuchangisha fedha za ujenzi wa Kanisa la KKKT Usharika wa Mwenge.
*************************************
NA MWANDISHI WETU
KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mwenge, Dar es Salaam, limevuna zaidi ya sh. milioni 119 katika harambee iliyoendeshwa jana na Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa kuchangisha fedha za kumalizia ujenzi wa kanisa hilo.
Hadi mwisho wa harambee hiyo iliyofanyika kwa watu kuchangia papo hapo na kunadiwa vitu mbalimbali, zilipatikana sh. 119,562,300 zikiwemo fedha taslim sh. milioni 30.7 ambazo Lowassa alichanga papo hapo kwa kumkabidhi Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi hiyo George Fupe.
Mapema katika risala, Mchungaji Luhuvilo Sigala alisema, ili kumalizia ujenzi wa kanisa hilo zilikuwa zinahitajika sh. milioni 94 na kwamba hadi sasa kanisa hilo limeshajengwa kwa asilimia zaidi ya 80.
Baadhi ya vitu vilivyonadiwa na Lowassa ambnaye alaifuatana na Mkewe, Regina Lowassa, ni mbuzi watano waliotolewa na waumini, mchele, sukari na mikungu ya ndizi.
Akizungumza katika misa kabla ya harambee hiyo, Fupe aliwataka waumini wa Kikristo na hususan wa KKKT kuhakikisha wanawalea watoto wao katika mazingira ya kupenda dini ili kuweza kupatikana waumini wa baadae.
Fupe alisema kujenga makanisa bora bila kuwalea watoto katika malezi hayo hakutakuwa na faida yoyote kwa sababu baada ya miaka ijayo yatabakia makanisa mengi yasiyo na waumini.
"kuna nchi nilitembelea hivi karibuni nikashangaa kuona makanisa makubwa makubwa, nilipohudhuria misa na kuombwa kuiendesha nilishangaa kukuta kanisa kubwa lakini ndani mna waumini wachache mno" alisema Fupe na kuongeza,
"Nikauliza mbona kanisa ni kubwa mno tena la ghorofa lakini waumini wachache? nikaambiwa siku hizi waumini hawaji kanisani na sababu kubwa ni kwamba vijana wamenyimwa utamaduni wa kuabudu walipokuwa watoto", alisema.
No comments:
Post a Comment