Shirikisho la Mpira wa Miguu la Morocco (FRMF) limehamisha mechi ya kundi D ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Morocco kutoka Casablanca na sasa itachezwa Marrakech.
Mechi hiyo itachezwa saa 1.30 jioni Oktoba 9 mwaka huu. Pia Algeria na Jamhuri ya Afrika ya Kati ambazo ziko kundi hilo zitacheza Oktoba 9 mwaka huu na muda huo huo ili kuepuka kupanga matokeo. Mechi hiyo itachezwa jijini Algiers.
Kwa vile hakuna mashirika ya ndege ya kimataifa yanayokwenda Marrakech, FRMF ndiyo itakayogharamia usafiri wa Taifa Stars kutoka Casablanca hadi Marrakech. Kwa mashabiki wa Tanzania wanaotaka kwenda kuishangilia Taifa Stars nauli kwa ndege za Morocco kutoka Casablanca- Marrakech- Casablanca ni dola 120.
Waamuzi wa mechi kati ya Stars na Morocco watakuwa Gassama Bakary, Jawo Dickory, Touray Sulayman na Camara Bakary, wote kutoka Gambia. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Zoumaro Gnofame kutoka Togo.
Kocha Jan Poulsen anatarajia kutangaza kikosi Septemba 26 mwaka huu kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco na kitaingia kambini Septemba 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment