Habari za Punde

*WALIOCHAKACHUA TIKETI ZA YANGA NA AZAM 'MBARONI'

UWANJA WA TAIFA ULIOTUMIKA KWA MECHI YA YANGA NA AZAM MWISHONI MWA WIKI ILIYOPITA.
Mmoja wa wauzaji tiketi kwenye mechi ya Azam na Yanga iliyochezwa Septemba 18 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Seleman Masoud aliripoti kupotelewa kitabu kimoja cha tiketi mara baada ya ugawaji wa vitabu hivyo kwa wauzaji kufanyika asubuhi ya siku ya mchezo kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Tiketi kutoka kwenye kitabu hicho ziliuzwa kwa mashabiki ambao miongoni mwao walikamatwa. 

Baada ya kukamatwa kwa kutiliwa mashaka walitakiwa kuonesha mahali ambapo wameuziwa tiketi hizo ambapo walionesha kwa muuzaji mwingine Salum Abdallah. 

Abdallah pia alikuwa ni mmoja kati ya wauzaji wa tiketi hizo katika mechi hiyo.

Wauzaji wote wawili walikamatwa na TFF na tukio kuripotiwa Kituo cha Polisi Chang’ombe siku hiyo.

Tukio hilo lilifunguliwa jalada namba CHA/IR/6257/2011 ambapo watuhumiwa wameshachukuliwa maelezo yao. 

Kitabu kilichoibwa kilikuwa na tiketi 100 zenye thamani ya sh. 300,000. Thamani ya kila tiketi ni sh. 3,000.

POULSEN KUTAJA TIMU SEPT 26
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen anatarajia Septemba 26 mwaka kutaja wachezaji watakaoingia kambini kwa ajili ya mechi dhidi ya Morocco itakayochezwa Oktoba 9 mwaka huu jijini Casablanca.

Timu inatarajia kuingia kambini Septemba 28 mwaka huu, na inatarajia kuondoka Oktoba 6 mwaka huu kwenda Casablanca. 

Mechi hiyo ni ya mwisho hatua ya makundi kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Equatoria Guinea na Gabon.

Poulsen ambaye pia ni Mkufunzi wa Makocha wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yuko nchini Gambia ambapo anaendesha kozi ya wakufunzi na anatarajia kurejea nchini Septemba 24 mwaka huu.

LIGI DARAJA LA KWANZA
Ligi Daraja la Kwanza inayoshirikisha timu 18 inatarajia kuanza mwezi ujao. Kamati ya Mashindano inayoongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa TFF, Ramadhan Nassib inatarajia kukutana Septemba 24 mwaka huu kuangalia mambo mbalimbali ya ligi hiyo.

Moja ya mambo ambayo kamati hiyo itafanya ni kupitisha tarehe ya kuanza ligi hiyo pamoja na vituo.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.