SHIRIKA la kutetea haki za kibinadam la 'Human Rights Watch', limetoa wito kwa Baraza la Mpito nchini Libya, NTC kuagiza makundi yaliyojihami kuacha kuwakamata watu kiholela na kuwahujumu wafungwa nchini humo.
Shirika hilo lilitembelea magereza 20 na kusema kuwa limepokea ripoti kuwa wafungwa sita waliteswa katika vituo vinavyosimamiwa na wanajeshi watiifu kwa Baraza la Mpito NTC.
Walinzi katika vituo hivyo wanatuhumiwa kuwadhulumu wafungwa katika magereza hayo ya muda kwa kuwapiga viboko na hata kuwatesa kwa kutumia umeme.
Aidha Shirika hilo linasema wafungwa wanaotuhumiwa kuhusika na visa vya ubakaji na mauaji walionekana kudhulumiwa zaidi na kushurutishwa kukiri mashtaka dhidi yao na walinzi katika magereza hayo.
Shirika hilo la 'Human rights watch', limetoa wito kwa Baraza hilo la Mpito, kubuni mfumo wa haki ambao utahakikisha kuwa wafungwa wote wanapewa haki sawa za kibinadamu.
No comments:
Post a Comment