MTUNISHA misuli maarufu wa Tanzania, David Nyombo anaondoka (kesho jumatano) kwenda Mumbai, India kushindana katika taji la dunia la Mr. Universe.
Nyombo ambaye mwaka jana alimaliza nafasi ya nne katika mashindano ya Anold Classic nchini Marekani, amesema kuwa amejiandaa vilivyo tayari kurejea na ushindi hapa nyumbani.
Alisema kuwa mashindano hayo yanayofanyika kuanza Novemba 3 mpaka 7, yatashirikisha zaidi ya watunisha misuli 180 kutoka nchi mbali mbali Duniani.
“Nimejiandaa vilivyo kwa ajili ya mashindano haya, nimetumia fedha zangu mwenyewe na msaada kutoka kwa marafiki zangu, lengo langu kubwa ni kuitangaza nchi nje ya mipaka na si vinginevyo,” alisema Nyombo.
Alisema kuwa pamoja na wadhamini wengi kushindwa kumsaidia, anashukuru juhudi zake zimefanikiwa na sasa anakwenda kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya mipaka.
“Ningeweza kusema sina fedha, watu wangenielewa japo nusu nusu, lakini nikaona kuwa fedha si kikwazo kwangu, najua watu watanipongeza mara nitakapofanya vizuri kama ilivyokuwa katika mashindano ya nyuma,” alisema Nyombo ambaye mwaka 2009 alishinda taji la Mr. Afrika.
Alisema kuwa anajua kuna ushindani, lakini yeye amejidhatiti zaidi katika uzani wa welter na bila shaka anaibuka kidedea.
Alisema kuwa katika mashindano ya mwaka jana nchini Baku, alibuka dani ya 12 bora, na katika mashindano yaliyofuata, alifanya vizuri zaidi na hicho ndicho kigezo cha kumwezesha kufanya vyema.
Mbali ya kushindana, Nyombo pia ataiwakilisha nchi katika mkutano wa mwaka wa Shirikisho la Mchezo huo Duniani, IFBB akiwa kama mjumbe.
No comments:
Post a Comment