Habari za Punde

*NADIR HAROUB 'CANAVARO' AONDOLEWA TAIFA STARS

Beki wa kati wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Nadir Haroub 'Canavaro' ameondolewa katika kikosi cha timu ya Taifa kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena.

Haroub ameondolewa baada ya kuumia kifundo cha mguu wa kulia (right ankle) akiwa mazoezini jana asubuhi (Novemba 5 mwaka huu).

Kwa mujibu wa daktari wa Stars, Dk. Juma Mwankemwa, mchezaji huyo hakuvunjika isipokuwa amepata mshtuko mkubwa wa kifundo hicho ambapo itamchukua wiki mbili kupona sawa sawa.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen amesema kutokana na hali hiyo Haroub hatakuwemo kwenye kikosi hicho kwa ajili ya mechi hiyo na ile ya marudiano ambayo itachezwa Novemba 15 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Poulsen amesema kwa muda uliobaki hataita mchezaji mwingine kwa ajili ya kuziba pengo la Haroub, hivyo kwa sasa atabaki na kikosi cha wachezaji 21 alionao kambini katika hoteli ya New Africa.

LESENI ZA UKOCHA ZA CAF DARAJA C
Kozi ya ukocha kwa ajili ya kupata leseni za daraja C kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itafanyika ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuanzia kesho (Novemba 7 mwaka huu) hadi Novemba 20 mwaka huu.
Makocha 30 ndiyo wanaoshiriki kozi hiyo itakayoendeshwa na wakufunzi wanne; Jan Poulsen kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Kasimawo Laloko (Nigeria) na Sunday Kayuni wanaotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Kim Poulsen kutoka Chama cha Mpira wa Miguu Denmark (DBU).
Washiriki wa kozi hiyo ni Abdul Nyumba, Absolom Mwakyonde, Ahmed Mumba, Christopher Eliakim, Dismas Haonga, Edward Hiza, Eliasa Thabit, Emmanuel Massawe, Fulgence Novatus, Gabriel Gunda, Gideon Kolongo, Haji Amir na Hassan Banyai.
Wengine ni Juma Mgunda, Jumanne Ntambi, Keneth Mkapa, Leonard Jima, Maarufu Yassin, Maka Mwalwisi, Mecky Maxime, Mohamed Tajdin, Mussa Furutuni, Mussa Kamtande, Peter Mhina, Richard Kabudi, Sebastian Nkoma, Stephen Matata, Tiba Mlesa, Wane Mkisi na Wilfred Kidau.
STARS KWENDA CHAD NOVEMBA 9
Timu ya Taifa Stars itaondoka nchini Novemba 9 mwaka huu kwenda N’Djamena, Chad kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayochezwa nchini humo Novemba 11 mwaka huu.

Msafara wa timu hiyo utakaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella utaondoka saa 9 kamili alasiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo utawasili N’Djamena saa 1 jioni ambapo Tanzania itakuwa saa 3 usiku.
Timu itarejea nchini Novemba 12 mwaka huu kwa ndege ya Ethiopian Airlines na kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi ya marudiano itakayochezwa Novemba 15 mwaka huu.
Powered by Sorecson : Creation de site internet
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF)

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.