Habari za Punde

*JERRY MURO NA WENZAKE WASHINDA KESI ILIYOKUWA IKIWAKABILI

Jerry Muro na mke wake wakitoka mahakamani baada ya kuachiwa huru jana.

Na Mwandishi wetu, Jijini Dar
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imewaachia huru kwa mashitaka yote matatu yaliyokuwa yakiwakabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Jarry Muro, Edmond Kapama pamoja na Deogratius Mgasa.

Hakimu aliyekuwa akiendesha kesi hiyo, Frank Moshi, alisema anawaachia washitakiwa hao baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao.

Muro, Edmond Kapama pamoja na deogratius Mgasa walikuwa wakikabiliwa na kesi ya kuomba na kutaka kupokea rushwa ya Sh. milioni 10 toka kwa aliyekuwa Muhasibu wa Wilaya ya Bagamoyo Michael Wage.

Mashitaka yao yalikuwa ni ya kula njama, kuomba rushwa na kujitambulisha kuwa maofisa wa TAKUKURU shitaka ambalo zaidi liliwakabili Mgasa na kapama.

Muro baada ya kutoka Mahakamani hapo alitangaza kwa wanahabari kuwasamehe wabaya wake wote ambao ni viongozi wa Serikali na baadhi ya maofisa wa Polisi na kuwataka waandishi wa habari kushikamana kuendelea kuibua uozo unaoendelea bila woga.

Katika hukumu hiyo, Hakimu Moshi, alisema baada ya kuangalia upande wa ushahidi mahakama ilikuwa na maswali ya kujiuliza kama upande wa Jamhuri uliweza kuthibitisha mashitaka dhidi ya washitakiwa ambapo shitaka la kula njama kwa nia ya kuomba rushwa ambalo linawahusu washitakiwa wote.

Shahidi huyo wa tatu wa Jamhuri, lisema kuwa alikutana na Muro kwenye mgahawa wa Califonia ambapo mawasiliano kati yao yaliendelea kwa njia ya simu ya mkononi.

Ushahidi huo ulikuwa hafifu kwasababu upande wa mashitaka haukuweza kuwasilisha karatasi ya mawasiliano kati yao kutoka kwenye kampuni ya mtandao wa simu (printout).

Aidha alisema kuwa picha za CCTV iliyowasilishwa mahakamani hapo ilikuwa ni kivuli kisichoonyesha sura za watu badala yake wangeleta CD na kuonyesha kwenye video ili watu waweze kutambulika kwa urahisi.

"Mawasiliano ni jambo la msingi kwasababu ili kula njama ni lazima mawasiliano yafanyike hivyo kuna mapungufu makubwa katika shitaka hilo". alisema Hakimu 

Dereva aliyemwendesha Wage alidaiwa kuwa na Wage pale mgahawa wa Califonia walipokutana na Muro, alitakiwa kuletwa athibitishe kama Wage na Muro walikutana upande wa mashitaka hawakumwita shahidi huyo.

Katika shitaka la kuomba rushwa lililowakabili wote katika ushahidi wake Wage, alieleza Muro na wenzake walimtaka awapatie Sh milioni 10 watamsaidia kwenye tuhuma zinazomkabili lakini hakuwa nazo akawapa sh milioni moja mbali na ushahidi huo hakuna ushahidi mwingine wa Serikali unaoonyesha kuwa walipokea fedha hiyo.

“Mahakama ilitegemea kuwapo na ushahidi wa mawasiliano kama haupo wa kuona lakini yote hayo hayakufanyika,” alisema hakimu Moshi.

Aidha hakimu alihiji kuwa Muro alikamatwa ndani ya gari, mahakama haielewi ni kwanini kulikuwa na haraka ya kufanya hivyo ni kwanini asingeachwa wakakutana na Wage ndipo akamatwe?, Kwa upande wa hotel ya Sea Cliff ni sehemu ya watu wa aina zote wanaotembelea na kuingia katika hoteli hiyo.

Washitakiwa Mgasa na Kapama hakimu Moshi, alisema hawakukamatwa eneo la tukio walikamatwa na kuunganishwa na halikufanyika gwaride la kuwatambua na cheti kuletwa mahakamani.

Shitaka linalowakabili Mgasa na Kapama la kujitambulisha maofisa wa TAKUKURU mahakama ilisema halikuthibitishwa lina mashaka. Alisema washitakiwa walijitambulisha kuwa mmoja anaitwa Dr na mwingine Musa.

Kwa upande wa mashitaka ulitakiwa kufuatilia mtaani kama majina hayo washitakiwa walikuwa wakiyatumia lakini hilo halikufanyika.

“Wage kama msomi ngazi ya uhasibu aliwezaje kukubali mtu ajitambulishe kwa mdomo kama ni Ofisa wa TAKUKURU bila kuonyeshwa Kitambulisho na akakubali? mahakama inapata mashaka”.

Aliongeza hakimu huyo kuwa  hakuna vielelezo na ushahidi wa kuthibitisha bila kuacha shaka hivyo washitakiwa wanaachiwa huru kwa mashitaka yote.

Aliendelea kusema kuwa risiti, pingu na miwani havikuwa na mgogoro katika kesi na kwa vile vilipatikana kwa risiti basi arudishiwe muhusika na upande unaotaka kukata rufaa wana ruhusiwa kufanya hivyo.
 Wakili kiongozi wa kesi hiyo Boniface Stanslaus, alisema taafifa atampelekea Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) ataamua kama watakata rufaa ama la.

Washitakiwa walifikishwa mahakamani Februari 5 mwaka jana kwa mara ya kwanza mbele ya Hakimu mkazi, Gabriel Mirumbe na kuachiwa huru jana Novemba 30, 2011.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.