Habari za Punde

*SERIKALI KUJENGA DARAJA KUBWA ZIWA VICTORIA - WAZIRI MAGUFULI

Na Mwandishi Wetu, Bunda
SERIKALI kupitia Wizara ya Ujenzi imesema, inatarajia kujenga daraja kubwa katika Ziwa Victoria kutoka Kisorya Bunda mkoani Mara, hadi Lugezi Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, ili kurahisisha usafiri kwa wananchi wa maeneo hayo.

 Kauli hiyo imetolewa jana na Waziri wa Ujenzi, Dkt. John Pombe Magufuli, wakati alipokuwa akizindua kivuko cha Mv. Ujenzi kinachotoa huduma kati ya wilaya ya Ukerewe, Mwanza na Bunda mkoani Mara.

Kivuko hicho cha Mv. Ujenzi chenye uwezo wa kubeba tani 8, kimejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Serikali ya Tanzania, na kimegharimu sh. Bilioni 2.4, na kwamba kina uwezo wa kubeba abiria 330 na kati yake, abiria 100 wanakaa kwenye viti pamoja na kubeba magari 10 kwa wakati mmoja.

Kwa mujibu wa Waziri Magufuli, mkakati huo utatekelezwa kwa miaka kadhaa ijayo, na kwamba vivuko vinavyotoa huduma ya kusafirisha abiria katika eneo hilo vitapelekwa maeneo mengine ambapo hakuna huduma kama hiyo muhimu, lengo ni kuondoa kero ya usafiri kwa Watanzania.

"Mipango ya baadaye ya Serikali ni kujenga daraja katika eneo hili la Ziwa. Tukikamilisha ujenzi huu wa daraja vivuko vyote viwili vya hapa tutavipeleka maeneo mengine ya nchi ambapo hakuna huduma hiyo.

"Huu ni mkakati mzuri wa Serikali ya CCM. Tukilijenga hili daraja, wapinzani nao watapita hapa, na hata wale wanaoandamana nao watatumia vivuko hivi vilivyotengenezwa na Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete", alisema Waziri Magufuli ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Chato mkoani Kagera .

Magufuli, alisema kuwa  "Kama tumepata jeuri ya kujenga daraja katika mto Malagarasi tutashindwa daraja hili la urefu wa kilometa nane?. Serikali ya CCM ipo kwa maslahi ya Watanzania, inatekeleza vizuri ilani yake na haishindwi kitu" alisema.

Iwapo Serikali itafanikiwa kujenga daraja katika eneo hilo kati ya Kisorya Bunda na Lugezi Ukerewe, itakuwa ni la kwanza kujengwa katika Ziwa Victoria, na kwamba mikakati hiyo ni vema ikatekelezwa na si kuishia kutoa maneno ambayo yatakuja kuwaudhi Watanzania.

Waziri Magufuli alipiga marufuku Halmashauri zote nchini kutoza ushuru kwenye vivuko vilivyojengwa na Serikali Kuu, na kuitaja Halmashauri ya wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kwamba inafanya wizi kwa kutoza ushuru katika kivuko cha Serikali cha Kigongo Ferri, na kwamba tabia hiyo ife kuanzia sasa.

Kuhusu ujenzi wa barabara ya lami kutoka Kisorya Bunda hadi Ukerewe mjini, yenye urefu wa kilometa 118.67, alisema itajengwa na kukamilika kabla ya mwaka 2015, na kwamba kwa sasa kampuni ya Intacco inaendelea na zoezi la upimaji barabara hiyo kwa gharama ya sh. milioni 650.

"Barabara hii tutaiwekea lami kabla ya Uchaguzi wa mwaka 2015. Hapa wapinzani msije kusema mmeijenga ninyi, maana ninyi hamna  Serikali inayofanya mambo mazuri haya ni yetu ya CCM", alitamba Waziri Magufuli katika uzinduzi huo wa Kivuko cha Mv. Ujenzi ambayo ni utekelezaji wa ahadi ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa mwaka 2007.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.