Habari za Punde

*SIMBA KUKIPIGA NA MTIBWA SUGAR MCHEZO MAALUM WA KUUAGA NA KUUKARIBISHA MWAKA 2012

Mashabiki wa Simba, wakishangilia katika moja ya mchezo wa timu yao Uwanja wa Taifa.

KLABU ya soka ya Simba itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Mtibwa Sugar ya Morogoro katika pambano litakalofanyika katika Uwanja wa Azam, Chamazi jijini Dar es Salaam JIONI ya Jumamosi, Desemba 31 mwaka huu.

Pambano hilo litakuwa la mwisho kwa Simba kucheza jijini Dar es Salaam mwaka huu. Pambano hilo pia litakuwa la mwisho kwa Simba kabla haijakwenda Zanzibar kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyopangwa kuanza Januari 2 mwakani.

Simba itaondoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar Januari Mosi mwaka huu (Jumapili).

Pambano dhidi ya Mtibwa litakuwa sehemu ya maandalizi ya michuano ya Mapinduzi, Ligi Kuu ya Tanzania na michuano ya kimataifa ambayo Simba itashiriki mwakani.

Mechi hiyo itakuwa ya kwanza kwa Kocha Mkuu wa Simba, Profesa Milovan Cirkovic, kukaa kwenye benchi la ufundi na kuiongoza klabu yake hiyo ambayo ni mabingwa watetezi wa Kombe la Mapinduzi na mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

Viingilio katika pambano hilo vitakuwa ni Sh 5,000 kwa VIP na 2,000 kwa majukwaa mengine. Simba imeweka kiingilio hicho ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kuhudhuria pambano hilo na kusherehekea kumaliza mwaka salama huku wakiitazama soka la uhakika.

Profesa Cirkovic ameahidi kwamba kwenye pambano hilo atashusha kikosi kamili cha wachezaji wa Simba ili kubaini ni kwa namna gani wachezaji wake wameyaelewa mafunzo yake.

“Nawakaribisha wapenzi na wanachama wa Simba na wapenda soka kwa ujumla waje kwa wingi kuiona Simba ikicheza. Nimesikia kwamba uwanja wa Azam ni mzuri na utaendana na aina ya mchezo ambao Simba itakuwa ikiucheza chini yangu. Nataka kuonyesha soka la asili la Simba,” alisema.






No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.