Habari za Punde

*USAJILI MASHINDANO YA KLABU BINGWA AFRIKA 'CAF' UNAENDELEA


ZOEZI la usajili kwa ajili ya timu za Tanzania zitakazoshiriki michuano ya ngazi ya klabu Afrika inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) linaendelea.
Yanga itacheza Ligi ya Mabingwa (CL) wakati Simba itashindana katika michuano ya Kombe la Shirikisho (CC). Kwa upande wa Yanga hadi sasa imeshawasilisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) majina ya wachezaji 28 wakati Simba majina 24 kwa ajili ya usajili huo.
Mwisho wa kufanya usajili ni Desemba 31 mwaka huu, na kila klabu inaruhusiwa kusajili hadi wachezaji 30. Hata hivyo Agosti mwakani kutakuwa na usajili wa dirisha dogo kwa timu ambazo hazikumaliza nafasi zote 30.
Kuna mifumo miwili ya usajili; online (mfumo wa mtandao) au offline (kutuma fomu za usajili CAF kwa njia ya DHL). TFF tumeamua kutumia mfumo wa online.
FIFA YAMTEUA MINJA KUSIMAMIA MECHI
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemteua Katibu wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Joan Minja kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia kati ya Zambia na Botswana.
Mechi hiyo ya raundi ya awali kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Wasichana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Azerbaijan itachezwa kati ya Februari 3, 4 au 5 mwakani jijini Lusaka.
Kwa upande wa Afrika nchi ambazo zitacheza raundi ya awali ya michuano hiyo ni Afrika Kusini, Botswana, Cameroon, Gambia, Ghana, Guinea, Namibia, Nigeria, Sierra Leone, Tunisia na Zambia.
KOZI YA MAKAMISHNA KUANZA KESHO
Kozi kwa ajili ya makamishna wa mechi za Ligi Kuu na mashindano mengine yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inafanyika kesho (Desemba 28 mwaka huu) na keshokutwa (Desemba 29 mwaka huu).
Washiriki wa kozi hiyo itakayofanyika ofisi za TFF ni wale wanaoomba kwa mara ya kwanza (beginners), na waliokosa ile ya awali iliyofanyika Agosti 6-8 mwaka huu. Pia ambao hawakufaulu katika kozi ya awali wanayo fursa ya kushiriki ya sasa.
Washiriki wanatakiwa kuwa waamuzi wastaafu na viongozi (administrators) wa mpira wa miguu katika ngazi mbalimbali. Pia wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao halisi (original) vya elimu.
Kutakuwa na mitihani ya kuandika ya sheria za mpira wa miguu na picha (video clips). Kwa wanaotaka kuwa makamishna ni lazima washiriki katika kozi ambapo ada ni sh. 10,000.
Makamishna waliofaulu kwenye kozi iliyopita ni Abdallah Mitole, Amri Kiula, Arthur Mambeta, Charles Komba, Charles Ndagala, David Lugenge, Edward Hiza, Fulgence Novatus, Gabriel Gunda, George Komba, Godbless Kimaro, Hamis Kissiwa, Hamis Tika, James Mhagama, Jimmy Lengwe, Michael Bundara, Mohamed Nyange, Mwijage Rugakingira, Omari Mwamela, Paul Opiyo, Pius Mashera, Salim Singano, Victor Mwandike na William Chibura.
Powered by Sorecson : Creation de site internetBoniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.