Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania imepokea kwa masikito makubwa taarifa za mafuriko na kusababisha maafa yaliyoukumba mkoa wa Dar es salaam na kugharimu maisha ya watu kufutia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha mkoani humo na sehemu nyengine za nchi.
Hali hii inatoa uhitaji wa taifa kushikamana na kukaa pamoja katika kuwafariji wafiwa na wale ambao walioguswa na athari za maafa hayo kwa namna moja ama nyingine.
“Tunafuatilia kwa karibu taarifa za maafa haya,
Tumeguswa na vifo vya watanzania wenzetu waliopoteza maisha na tunatoa pole kwa wafiwa na tunawafariji wote waliothiriwa na maafa haya”alisema Ofisa Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Vodacom Tanzania Mwamvita Makamba.
Vodacom tayari imeshachukua hatua za awali za dharura kusaidia waathirika na itatumia shilingi Milioni 30 kutoka mfuko wake wa kusaidia jamii wa Vodacom Foundation.
“Kwa sasa tunafanya mawasiliano na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambae ndie Mwenyekiti wa Kamati ya Maafa kupata mahitaji muhimu ya haraka ili tuweze kutumia fedha hizo. Tunatarajia kukamilisha mchakato huu kwa haraka iwezekanavyo kutoa unafuu wa maisha kwa waathirika.”Amebainisha Mwamvita
Aidha kampuni hiyo imetangaza pia fursa kwa wateja wake kuungana na Menejimenti na wafanyakazi wake kuonesha kuguswa kwao kwa kuchangia walichonacho kupitia nambari maalum ya maafa ya Vodacom Red Alert na kwa njia ya m-pesa.
Kupitia nambari ya Red Alert 15599 mteja anaweza kuchangia shilingi 500 kwa kutuma ujumbe mfupi – SMS wenye neno MAAFA na hakuna ukomo wa ujumbe na kwa njia ya m-pesa mteja anaweza kuchangia kuanzia shilingi 1,000 na zaidi kwenda nambari 155990.
“Tunaimani kuwa wote kwa pamoja tutaonesha umoja, upendo na mshikamano wetu wa kitaifa unaojenga tunu ya utanzania wetu kusaidia wenzetu ambao kwa wakati huu wapo katika mashaka makubwa wakihitaji faraja ya kila aina”. Amesema Mwamvita.
Michango yote itakayokusanywa kupitia nambari hizi itawasilishwa kwa kamati ya Maafa ya mkoa kuongeza Nguvu katika juhudi za kuwasaidia waathirika na kwamba utaratibu wa kuwapatia taarifa wachangiaji utakuwepo.
Aidha kampuni ya Vodacom Tanzania inavipongeza kipekee vyombo vya ulinzi na usalama nchini kwa juhudi kubwa za uokozi kwa kushirikiana na wananchi hatua ambayo bila shaka imesaidia kunusuru maisha ya maelfu ya watu.
No comments:
Post a Comment