Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akizungumza na waandishi wa habari leo katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, Dar es Salaam, kuhusu maandaizi ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa CCM ambayo yataanza mwanzoni mwa mwezi Februari na kufikia kilele chake Februari 5, 2012.
Nape alisema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitatumia maadhimisho hayo ya mwaka huu pamoja na mambo mengine kupiga vita wagombea wote wanaotoa na kupokea rushwa.
Pia kitatumia maadhimisho hayo kuhamasisha wananchama wake waadilifu na waaminifu kujitokeza kugombea katika uchaguzi huo utakaofanyika mwaka huu, kuanzia ngazi za mashina hadi taifa.
Aidha Nape alisema, Chama kitatumia fursa hiyo pia kuwaelimisha wanachama wake na wananchi kwa ujumla kuhusu mabadiliko ya Katiba ya nchi yanayokusudiwa kufanyika, ikiwa ni pamoja na msimamo wa kuilinda nchi, amani, na kupatikana kwa Katiba bora itakayokuwa na manufaa kwa watu wote.
"maadhimisho hayo yataanza Februari mosi na kufikia kilele chake Februari 5, 2012 yakiambatana na shughuli mbalimbali yakiwemo matembezi ya mshikamano yatakayofanyika kila mkoa wakati Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete atakuwa mgeni rasmi katika kilele cha matembezi hayo kitakachofanyika Mwanza". alisema Nape .
"Maadhimisho haya ni kumbukumbu muhimu kwa Chama Cha Mapinduzi kutimiza miaka 35 ya uhai wake tangu vyama vya TANU na ASP vilipovunjwa na kuundwa chama kipya cha CCM chenye nguvu, Februari 5, 1977", aliongeza Nape
Alisema kwa kuwa mwaka huu ni wa Uchaguzi Mkuu wa Chama hivyo Chama kimependekeza kaulimbiu mahsusi itakayotumika katika sherehe hizo kuwa ni "CCM Imara na Madhubuti inaanza na mimi, naimarisha Chama Changu kwa kuchagua viongozi bora na waadilifu".
Nape alisema uzinduzi wa sherehe hizo utafanyika kila mkoa Januari 30, mwaka huu na kufuatiwa na wiki ya shughuli za Jumuia, ambazo kila Jumuia itapanga ratiba ya mikutano ya ndani na shughuli za kijamii kama kupanda miti.
CCM imewataka wajumbe wa Kamati ya Siasa na Halmashauri Kuu ya mikoa kutumia wiki hiyo kufanya ziara katika matawi kuimarisha uhai wa Chama.
No comments:
Post a Comment