Habari za Punde

*HAMAD RASHID NA WENZAKE WATATU WATIMULIWA CUF WAVULIWA UANACHAMA

Mbuge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid, akisherehekea katika mkesha wa sherehe za miaka 50 ya uhuru na Mbunge na Vijana wa CCM hivi karibuni.
***********************************************
WAJUMBE wanne wa Baraza Kuu la chama cha CUF akiwamo Mbunge wa Jimbo la Wawi, Hamad Rashid, wamefukuzwa na kuvuliwa uanachama wa chama hicho.

Akitangaza uamuzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) Julius Mtatiro, alisema kuwa Baraza Kuu la Chama hicho limefikia uamuzi wa kuwatimua viongozi hao baada ya kubainika wamepoteza sifa za uongozi na kutaka kukisaliti chama na kusababisha migogoro ndani baina ya wanachama.

Amesema Baraza kuu la CUF limewafukuza viongozi hao baada ya kupata baraka kutoka kwa kikao cha baraza Kuu hilo na kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa bara na theluthi mbili kutoka katika wajumbe wa baraza kuu la  Zanzibar.

Kwa mujibu wa Mtatiro,  kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe 56 ambao kati yao 47 ndio walipiga kura na kura mbili tu ndizo zilipinga maamuzi hayo.

Mtatiro aliwataja wengine waliofukuzwa kuwa ni, mjumbe wa baraza kuu la CUF Doyo Hassan Doyo kutoka  mkoa wa Tanga, Juma Sanani ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi, na Shoka Khamis Juma ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Micheweni kwa tiketi ya CUF kipindi kilichopita huku Yasin Mrotwa akipewa onyo kali kwa ajili ya chunguzwa.

Hatma ya wajumbe wengine itajulikana baadaye baada ya kujadiliwa na vikao mbali mbali vya chama cha CUF kwa sababu wengine ni wanachama wa kawaida na sio wajumbe wa baraza kuu ambacho ni chombo cha juu chenye maamuzi.

Akizungumzia hatua hiyo, Hamad Rashid,  amepinga uamuzi wa kufukuzwa katika chama cha CUF na kumuita Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa ni dikteta mkubwa na Uongozi asiyeheshimu maamuzi ya mahakama.

Kwa mujibu wa Hamadi Rashid, uamuzi huo umekuja wakati Hamad na wenzake wakiwa tayari wameweka pingamizi kutoka mahakama kuu kupinga maamuzi ya mkutano wa Baraza Kuu na hati ya mahakama ipo mikononi wa CUF.

Hamad alisema watakwenda tena mahakamani Februari 14 kusikiliza pingamizi la kikao hicho, ambapo hata hivyo alipoulizwa Mtatiro kuhusu hati ya mahakama kama wanayo alikataa na kusema hawakubaliani nayo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.