Habari za Punde

*JESHI LA POLISI IRINGA LAWAOMBA RADHI WAANDISHI WA HABARI

  Baadhi ya waandishi wa habari wa Iringa wakiwa katika kikao na Kamanda wa Polisi.
JESHI la polisi mkoa wa Iringa limemaliza tofauti zake na vyombo vya habari mkoani humo kwa kuwaomba radhi waandishi na kumlipa kamera mwandishi wa habari wa ITV Laurian Mkumbata aliyevunjiwa kamera yake na mmoja kati ya maofisa wa juu wa jeshi la polisi wilaya ya Iringa.

Mbali ya kuwaomba radhi waandishi waliopatwa na misukosuko na askari polisi wakati wakiwa katika kutimiza wajibu wao bado jeshi hilo la polisi kupitia kamanda wa polisi mkoa wa Iringa, Evarist Mangalla limeomba vyombo vya habari mkoani humo  kusamehe yale yote ya mwaka 2011 na kuuanza mwaka kwa kujenga mahusiano na jeshi la polisi huku akipiga marufuku askari wake kuwazuia waandishi wanapokuwa katika harakati za kuhabarisha umma .

Aidha jeshi hilo limejipongeza kwa kuimarisha ulinzi wakati wa sikukuu za kufunga na kuukaribisha mwaka mpya na kuwa hakuna uharifu wowote uliojitokeza katika kipindi chote cha sikukuu.

Kamanda Mangalla aliyasema hayo leo wakati wa kikao cha pamoja na vyombo vya habari na kupongeza utendaji kazi wa vyombo vya habari mkoani hapa katika kulisaidia jeshi hilo la polisi kutoa elimu kwa wananchi.

Alisema kuwa katika mkoa wa Iringa kwa kipindi hiki cha siku kuu ya Krisimas na mwaka mpya wananchi wake wamesherekea kwa amani na utulivu na kuwa hakukuwa na matukio ya kiuharifu ambayo yalipata kujitokeza katika sherehe hizo.

Hivyo alisema kuwa ni jambo la kujipongeza kuona kuwa wananchi wamefunga mwaka bila ya kusumbuliwa na waharifu hao na kuomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi katika kuwafichua waharifu na uharifu katika maeneo wanayoishi.

Kwani alisema kuwa kwa mwaka huu wananchi wa mkoa wa Iringa waliuanga na kuukaribisha mwaka kwa namna ya pekee tofauti na miaka mingine ambayo matukio ya watu kuchoma mataili na kufanya vurugu wakati wa mkesha huo huwa hutawala kwakiasi kikubwa .

Katika hatua nyingine kamanda huyo wa polisi aliwataka maofisa wake wa jeshi la polisi kuepuka kuwazuia waandishi wa habari wanapokuwa katika shughuli zake huku akisisitiza ushirikiano kati ya vyombo vya habari na jeshi la polisi.

Alisema kwa mwaka jana kulikuwepo kwa hali ya kutoelewana kati ya jeshi la polisi na vyombo vya habari baada ya baadhi ya waandishi kuzuiwa kufanya kazi yao na maofisa hao wa polisi na kuwa hategemei mwaka huu 2012 tofauti hizo zikaendelea kwa vyombo hivyo.

Kwa upande wake mwanahabari Mkutamba akizungumza katika kikao hicho alimpongeza kamanda huyo wa polisi kwa kupigania kulipwa kamera yake iliyovunjwa na mmoja kati ya askari wakati wa vurugu za misukule katika eneo la Frelimo mjini Iringa.

"Hakika nampongeza sana kamanda wa polisi kwa kunisaidia kupata kamera yangu ....nimeipata kamera yangu yenye thamani ya shilingi milioni 1.5 kweli nashukuru kamanda wa plisi na wanahabari wenzangu kwa kunipigania kupata haki yangu"


No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.