UONGOZI wa Klabu ya Mabingwa wa Soka nchini Yanga ya jijini Dar es Salaam kwa kushirikiana na Kampuni ya Clouds Media kupitia redio yake ya Clouds Fm, kwa pamoja wamezindua shindano la kutafuta wimbo maalumu wa Klabu hiyo utakaoshindaniwa na Wasanii mbalimbali hapa nchini na baada ya wimbo huo kupatikana utatumika katika mashindano mbalimbali pamoja na shughuli za klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mjumbe wa Kamati ya utendaji wa Klabu hiyo, Ally Mayai, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati inayosimamia zoezi zima la upatikanaji wa wimbo maalum wa Klabu hiyo, alisema kuwa uzinduzi huo umefanyika Januari 29 Mwaka huu jijini Dar es Salaam na unatarajiwa kukamilika Februari 7 Mwaka huu.
Katika kufanikisha zoezi hilo jumla ya nyimbo kumi bora zitachaguliwa na wanachama wa Klabu hiyo kwa ajili ya kupata wimbo mmoja ambao utakuwa ni maalumu ambao utatumika katika mambo mbalimbali ikiwemo michuano ya ndani nchi pamoja na ya kimataifa na shughuli za Kimaendeleo za Klabu ya Yanga. alisema Mayai.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo mara baada ya kupatikana kwa wimbo huo maalum Msanii na wimbo huo utatangazwa katika sherehe za 'Yanga Day' zinazotarajiwa kufanyika Februari 12 Mwaka huu jijini Dar es Salaam na mshindi aliyepatikana atakabidhiwa zawadi yake.
Klabu ya Yanga ni moja ya Klabu Kongwe hapa nchini hivi karibuni ilianzisha Kampeni ya kutafuta wimbo maalum kama utambulisho kwa wapenzi na wanachama wa Klabu hiyo.
Wimbo pekee ambao uliokuwa ukitumika katika shughuli mbalimbali zinazohusu klabu ya Yanga ni ule uliotungwa na Hayati Pepe Kalle usemao ''Yanga Afrika Yanga Afrika ni Mabingwa wa soka wa Afrika Mashariki na Kati'' ambao unatumika katika vituo mbalimbali vya radio hapa nchini.
No comments:
Post a Comment