Habari za Punde

*MGOMO WA MADAKTARI WAMALIZIKA KWA KATIBU MKUU NA MGANGA MKUU KUSIMAMISHWA KAZI

SERIKALI ya Tanzania imewasimamisha kazi Maofisa wa Ngazi za juu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika hatua muhimu ya kumaliza mgomo wa madaktari uliokuwa umeshik hatamu nchi nzima.

Akitangaza uamuzi wa serikali, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, aliyefika na kuzungumza na madaktari waliogoma, amewataja waliosimamishwa kazi mara moja kuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu Dk Deo Mtasiwa.

Aidha Waziri Mkuu alisema kuwa Katibu Mkuu na Mganga Mkuu wamesimamishwa kazi ili pia kupisha uchunguzi dhidi yao kwa kile kilichoelezwa kuwa pia wana tuhuma nyingine kinyume na maadili ya kazi.

Waziri Mkuu Pinda amesema wengine wanaotarajiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa kusubiri uamuzi wa Rais, ni pamoja na Waziri wa Afya Dk Haji Mponda na Naibu wake Dk Lucy Nkya.

Mgomo wa madaktari ambao umedumu nchini kwa takriban wiki tatu sasa umesababisha kuzorota kwa huduma mbalimbali katika hosptali za umma na nyingine kufunga vitengo muhimu na kusababisha vifo kadhaa vya watanzania waliokosa huduma.

Madaktari hao waligoma kwa kile walichodai kuwa wanadai nyongeza ya mishahara, mazingira mazuri ya kazi pamoja na marupurupu mengine ambapo serikali imekubali kuyashughulikia.

Katika makubaliano na Waziri Mkuu na madakatari waliogoma wamekubali kumaliza mgomo na Ijumaa yaani kesho, wanatarajiwa kurejea kazini na kuchapa kazi kama kawaida.

Miongoni mwa tuhuma zinazoelezwa kuwakabili Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Mganga Mkuu ni pamoja na kuwa na miradi ya kuwaingizia fedha na kuwa na makampuni yanayoendesha shughuli mbalimbali katika sehemu za Wizara hiyo na kile kilichodaiwa kuwa na kampuni inayoshina sare za wafanyazi kwa Sh. 600, 000 kila moja na miradi mingineyo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.