Mtihani wa uwakala wa wachezaji (players agent) wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Alhamisi ya Machi 29 mwaka huu saa 10 kamili asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kutakuwa na jumla ya maswali 20 kwenye mtihani huo, 15 yanatoka FIFA kuhusiana na kanuni za kimataifa za mpira wa miguu na matano yatatoka TFF kuhusiana na kanuni mbalimbali zinazotawala mchezo huo nchini.Kwa ambao wangependa kufanya mtihani huo utakaokuwa katika lugha ya Kiingereza wanatakiwa
kujisajili TFF kwa ada ya dola 50 za Marekani ambapo watapewa utaratibu na maeneo ambapo mtihani huo unalenga. Muda wa kufanya mtihani hautazidi dakika 90.
Mtihani uliopita ulifanyika Septemba 29 mwaka jana ambapo watahiniwa wanane walijitokeza na kufanya mtihano huo.
Mpaka sasa Tanzania ina mawakala saba wa wachezaji wanaotambuliwa na FIFA. Mawakala hao ni Ally Mleh wa Manyara Sports Management, Damas Ndumbaro, John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na Said Tully.
RAUNDI YA 16 LIGI KUU YA VODACOM
Mzunguko wa 16 wa Ligi Kuu ya Vodacom kuwania ubingwa wa Tanzania Bara unaanza kesho (Februari 4 mwaka huu) kwa mechi tatu. Coastal Union itakuwa mgeni wa Moro United kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Nayo Villa Squad itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Ruvu Shooting na Polisi Dodoma zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
Viingilio kwa mechi ya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vitakuwa sh. 3,000 kwa viti vya bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP B na C, sh. 15,000 kwa VIP A wakati Uwanja wa Chamazi ni sh. 10,000 kwa Jukwaa Kuu na sh. 3,000 mzunguko.
Kwa mechi ya Mlandizi kiingilio ni sh. 2,000 kwa mzunguko wakati Jukwaa Kuu itakuwa sh. 5,000.
Pia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko ya muda wa kuanza mechi za ligi hiyo kwa kituo cha Dar es Salaam. Mechi zinazochezwa wikiendi kwenye Uwanja wa Taifa zitaaza saa 10 kamili jioni wakati zile zinazochezwa siku za kazi zitaanza saa 10.30 jioni. Mechi zote za Uwanja wa Azam- Chamazi zitaanza saa 10 kamili jioni.
MZUNGUKO WA PILI LIGI DARAJA LA KWANZA (FDL)
Mzunguko wa pili (second leg) wa Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inayochezwa katika makundi matatu tofauti unaanza kesho (Februari 4 mwaka huu) kwa mechi sita.
Katika kundi A, Morani FC itakuwa mwenyeji wa Burkina Faso ya Morogoro katika mchezo utakaochezwa Kiteto mkoani Manyara. Kwa upande wa kundi B timu zote sita zitakuwa uwanjani.
Small Kids ya Rukwa itacheza na Polisi ya Iringa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Mbeya City na Tanzania Prisons zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya na Majimaji na Mlale JKT watapepetana katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Kundi C litaanza kwa mechi mbili ambapo AFC ya Arusha watakuwa wageni wa Manyoni mkoani Singida na Rhino na Polisi Tabora zitakwaruzana kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Mechi nyingine ya kundi hilo itakuwa kati ya 94 KJ na Polisi Morogoro ambayo itachezwa keshokutwa (Februari 5 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani.
No comments:
Post a Comment