Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
NA MAGRETH KINABO- MAELEZO
HOSPITALI ya Mwananyamala iliyopo jijini Dares Salaam inaendelea kutoa huduma za matibabu ya afya kwa wagonjwa licha ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kutangaza kuanza kwa mgomo katika hospitali za serikali.
Waandishi wa Idara ya Habari ( Maelezo) walitembelea hospitalini hapo na kushuhudia huduma zikiendelea kama kawaida, ambapo waliona madaktari na manesi wakitoa huduma kwa wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utoaji wa huduma, Katibu wa Afya wa hospitali hiyo, Edwin Bisakala alisema hali ni shwari.
“ Sisi hapa watumishi hawajagoma wanaendelea na kazi vizuri isipokuwa baadhi ya madaktari walio katika mafunzo ya vitendo.
Hapa madaktari walio katika mafunzo ya vitendo wapo 52 lakini walioripoti katika orodha ya daftari kuwa wako kazini leo ni 21, hata hivyo kutoripoti kwa baadhi yao hakuna madhara katika utendaji kazi,” alisema Bisakala.
Alifafanua kuwa wapo wengine 10 ambao ni kitengo cha macho na huduma za dawa ambao hawaripoti kwao ingawa wanafika kufanya mafunzo ya vitendo.
Aliongeza kuwa hata katika mgomo wa awali waliogoma walikuwa ni madaktari walio katika mafunzo ya vitendo.
Bisakala, alisema kuwa anashangazwa na kitendo cha baadhi ya madaktari walioko katika mafunzo ya vitendo kutoripoti wakati juzi na jana wamelipwa fedha zao kama kawaida.
Akizungumzia kuhusu mgomo huo alisema kuwa ni vizuri (sisi viongozi tukisikia matatizo tushukuru kwa kuyafahamu na kuyashughulikia na kutoa maamuzi haraka hata kwa kutoa madaraka kwa wengine (deligate power).
Alishauri kuwa serikali ifanye haraka ili kuweza kutangaza waraka wa posho ambao utaonyesha posho za zamani na mpya kwa watumishi wa sekta zote.
Waandishi hao pia walitembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Kitengo cha Taasisi ya Mifupa (MOI) ambapo asubuhi huduma zilikuwa zikiendelea kama kawaida.
Kwa upande wa hospitali ya Temeke waandishi walioshuhudia baadhi ya ndugu wa wagonjwa na wagonjwa wakiwa nje wakiwa wamesimama na wengine wamekata tamaa baada ya kutangazwa kwa mgomo huo majira ya mchana.
Na katika Hospitali ya KCMC mjini Moshi, Madaktari na Wauguzi, wao wamedai kuwa hawatagoma wala kuhusika na mgomo huo ulioitishwa na Chama cha Madaktari, kutokana na wao kuwa waelewa zaidi na kuiacha Serikali ijipange kutangaza mfumo mpya wa Posho.
''Kwani hata tukigoma tutaua watu bure ambao hawana hatia wakati tunaelewa wazi kuwa mwaka wa kifedha umeshapita na Serikali imeshatangaza kujipanga katika msimu ujao wa kifedha ili kurekebisha malalamiko yetu, sasa tunagoma tunamgomea nani''?, alihoji mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment