Habari za Punde

*KAMATI YA MISS TANZANIA YATOA KALENDA YA MABADILIKO YA MASHINDANO YA UREMBO YA DUNIA

 Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, akizunguma na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Mgahawa wa Hadees, leo kuhusu mabadiliko ya kalenda ya mashindano ya urembo ya Dunia na Miss Tanzania. Kulia ni Ofisa wa Kamati hiyo, Mr. Lameck Shah.
********************************************************************
*Kupeleka mwakilishi katika mashindano ya Dunia
*Mshiriki kupatikana kwa kufanyiwa usaili na mchujo kati ya warembo 10
KAMATI ya Miss Tanzania, leo imetoa rasmi mabadiliko ya Kalenda ya mashindano ya urembo ya Dunia, yanayoifanya Kamati hiyo pia kufanya mabadiliko ya mashindano yake ya Miss Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kamati ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga, alisema kuwa waandaaji wote wa mashindano hayo kutoka nchi mbalimbali walipewa taarifa hiyo ya mabadiliko ya mashindano ya uremo ya Dunia (Miss World) katika mkutano uliofanyika nchini Uingereza mwezi Novemba 2011.
Mashindano hayo ya urembo ya dunia yanatarajia kufanyika nchini China mwezi Agosti mwaka huu, badala ya mwezi Novemba na Desemba kama ilivyozoeleka, ambapo washiriki kutoka nchi mbalimbali watatakiwa wawe wameshafika nchini China mwezi Julai mwaka huu.
Kutokana  na mabadiliko hayo na utaratibu wa kumpata mrembo wa Tanzania atakayeiwakilisha Tanzania katika mashindano hayo, Kamati ya Miss Tanzania nayo imefanya mabadiliko ya mashindano yake, ambapo kwa mwaka huu italazimika kutuma mwakilishi atakayeshiriki katika mashindano hayo ya dunia ya mwaka huu.
Aidha Lundenga alifafanua jinsi ya kumpata  Mwakilishi  huyo na kusema kuwa atapatikana kwa njia ya kufanyiwa usaili, ambapo warembo wote watakaojitokeza katika usaili huo watafanyiwa mchujo na kupatikana jumla ya warembo 10 watakaopanda jukwaani katika Tafrija maalum iliyoandaliwa ili kumpata mwakilishi atakayeiwakilisha Tanzania katika fainali za mashindano hayo ya dunia.
Pia Lundenga aliweka wazi kuwa Katika mchakato huo mzima wa kumpata mshiriki wa mashindano ya urembo ya Dunia, hawatahusishwa Mawakala wa mashindano hayo.
Lundenga, aliwataka warembo wote wenye sifa na nia ya kushiriki katika mchujo huo wa usaili wawasiliane na Ofisi za Kamati ya Miss Tanzania au mawakala wa mashindano hayo walio katika mikoa yote ya Tanzania, ambapo watapatiwa maelekezo zaidi kuhusu ushiriki wa mchujo huo.
‘’Pamoja na mabadiliko haya ya mashindano ya Dunia, lakini mashindano ya Redd’s Miss Tanzania 2012, yataendelea katika ngazi zote kama kawaida na mshindi wa Redd’s Miss Tanzania 2012, ataiwakilisha Tanzania katika Fainali za mashindano ya urembo ya Dunia ya mwaka 2013, ambapo atakuwa na muda wa maandalizi ya miezi saba baada ya shindano’’, alisema Lundenga
Aidha alisema kuwa Fomu za kushiriki mchujo wa ‘Second Chance Min Compatition’ ili kumpata mwakilishi wa Dunia, zitaanza kutolewa kesho Machi 16, katika Ofisi za Kamati hiyo, zilizopo Mtaa wa Mkwepu jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.