Habari za Punde

*TFF KUWAENDELEZA WAAMUZI WATOTO WA TWALIPO

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaendelea na mpango wake wa kuwaendeleza waamuzi watoto wa Kituo cha Kambi ya Twalipo kilichoko Mgulani jijini Dar es Salaam kwa kuwapa mafunzo zaidi na kuwatumia katika mashindano mbalimbali.
 
Lengo ni kuboresha uwezo wao katika kuchezesha mchezo wa mpira wa miguu na kutoa changamoto kwa vijana wadogo wengine, hasa wa shule za msingi, sekondari na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kuingia katika uamuzi ili kujenga kizazi kipya katika fani hiyo.
 
Wazo la kuwa na waamuzi watoto lilianzia kwa Meja Bakari wa kituo hicho, juhudi ambazo TFF inazipongeza na kuziunga mkono kwa kutoa mafunzo zaidi kwa wahusika. Wiki mbili zilizopita tuliwaandalia mafunzo zaidi ya kuwanoa ambayo yaliendeshwa na Mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Leslie Liunda.
 
TFF imeshawatumia waamuzi hao watoto katika mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Kombe la Uhai), michuano ya vijana ya Rollingstone iliyofanyika jijini Arusha na fainali za Copa Coca-Cola. Mashindano yote hayo yalifanyika mwaka jana na kiwango walichoonesha waamuzi hao kilikuwa kizuri.
 
Hivyo tutaendelea kuwapa mafunzo zaidi na mashindano mengine kadri tutakavyoona inafaa kwa lengo la kuwajenga na kuwaongezea ujuzi.
 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.