MKUTANO MKUU WA MWAKA 2011 WA TFF
Mkutano Mkuu wa Mwaka (AGM) wa 2011 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) umefanyika kwa siku mbili (Aprili 21-22 mwaka huu) kwenye ukumbi
wa NSSF Waterfront na kuhudhuriwa na wajumbe 104. Mkutano ulipokea taarifa,
kufanya uamuzi katika masuala mbalimbali na mengine yaliyojitokeza kama
ifuatavyo;
EL MAAMRY, NDOLANGA WATUNUKIWA URAIS WA HESHIMA
AGM ilipitisha pendekezo la kuwatunuku urais wa heshima wa TFF, Alhaji
Said Hamad El Maamry na Muhidin Ahamadi Ndolanga lililowasilishwa na Mwenyekiti
wa mkutano huo ambaye pia ni Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Alhaji El Maamry ambaye ni mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) alikuwa Mwenyekiti wa TFF wakati huo ikiitwa Chama cha Mpira
wa Miguu Tanzania (FAT) kuanzia mwaka 1973 hadi 1986. Alhaji Ndolanga aliongoza
FAT kuanzia mwaka 1993 hadi 2004.
BAJETI YA MWAKA 2012
Bajeti ya Mwaka 2012 ya sh. 7,246,628,650 kwa ajili ya matumizi ya TFF
ilipitishwa. Kwa mwaka 2012 TFF inatarajia kukusanya sh. 7,572,991,433 kupitia
vyanzo mbalimbali.
Vyanzo hivyo ni viingilio vya uwanjani vinavyotarajiwa kuingiza asilimia
22 ya mapato yote, udhamini (asilimia 74) na vyanzo vingine kama haki za
matangazo ya televisheni, ada za ushiriki wa timu katika mashindano mbalimbali,
misaada kutoka FIFA na CAF ambayo kwa pamoja vinatarajiwa kuingiza asilimia nne
ya mapato yote.
KAMATI YA LIGI YA TFF
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) itaendelea
na mchakato wa kupendekeza mifumo mitatu tofauti ya chombo
kitakachosimamia/kuendesha Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Ligi Daraja la Kwanza
(FDL) ikieleza faida na athari za kila mfumo uliopendekezwa na baadaye
kuwafanya mawasilisho (presentation) kwenye Kamati ya Utendaji.
Baada ya kuwasilisha mifumo hiyo kwa Kamati ya Utendaji, Kamati ya Ligi
itapendekeza mfumo upi kati yao hiyo inaoona unafaa kabla ya kufanyika uamuzi
wa mwisho.
Lengo la kuunda chombo maalumu cha kuendesha ligi ni kuongeza ufanishi
katika uendeshaji wa VPL na FDL, na pia kuifanya Sekretarieti ya TFF
kushughulikia zaidi shughuli za maendeleo.
UUZWAJI WA TIMU
Uuzaji wa timu linabaki kuwa suala la kisheria. Lakini TFF imeweka
utaratibu ufuatao; lazima Mkutano Mkuu wa klabu husika uidhinishe uuzaji, na
timu ikishauzwa inabaki katika mkoa husika.
MFUMO WA MASHINDANO
Kwa vile kuna tatizo la ligi mbalimbali kuwa fupi, hali inayosababisha
baadhi ya wachezaji katika madaraja ya chini kucheza ligi zaidi ya moja katika
msimu mmoja, mfumo wa ligi/mashindano utaangaliwa upya.
Mfumo uliopo sasa uliwekwa kwa ajili ya kuvutia uwekezaji katika mpira
wa miguu ambapo mwekezaji anaweza kuanzisha timu, na ndani ya miaka mitatu
ikacheza Ligi Kuu. Pili, ilikuwa ni kuondoa mlolongo mrefu wa ligi, na
kuwafanya wanachama wa TFF (mikoa) nao kuendesha ligi zao mikoani.
Ijulikane kuwa ligi za mikoa (regional leagues) zinachezwa. Kwa sababu
TFF inaendeshwa kwa mfumo wa shirikisho (federation), nia ni wanachama wa
federation nao kuwa na majukumu ya kusimamia na kuendesha ligi, kwa vile TFF
haiwezi kusimamia ligi zote.
MAREKEBISHO YA KATIBA
Mkutano Mkuu wa TFF umepitisha marekebisho ya Katiba katika maeneo
mawili; moja ni kuanzisha Baraza la Wadhamini ambalo linatakiwa kuwa na wajumbe
wasiopungua watatu na wasiozidi watano.
Marekebisho mengine ni kuongeza idadi ya kanda kutoka kumi na moja za
sasa hadi 13. Marekebisho hayo yamefanyika kutokana na Serikali kuongeza mikoa
mipya ya kijiografia.
Kanda mpya sasa zitakuwa Kagera/Geita, Arusha/Manyara,
Kilimanjaro/Tanga, Katavi/Rukwa, Njombe/Ruvuma, Dodoma/Singida, Dar es Salaam,
Shinyanga/Simiyu, Mwanza/Mara, Lindi/Mtwara, Kigoma/Tabora, Mbeya/Iringa na
Pwani/Morogoro.
Ukiondoa mamlaka ya uteuzi aliyonayo Rais kwa mujibu wa Katiba ya TFF,
wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji huchaguliwa kwa kanda.
HESABU ZILIZOKAGULIWA
Mkutano Mkuu ulipitisha hesabu zilizokaguliwa za mwaka 2010 (Audited
Accounts) , na pia kuiteua kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya TAC Associates kuwa
mkaguzi wa hesabu za TFF kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
YANGA YAOMBA RADHI MKUTANO MKUU
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga ambaye pia mjumbe wa Mkutano Mkuu
wa TFF akiwakilisha klabu za Mkoa wa Dar es Salaam, Mohamed Bhinda aliwaomba radhi
wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kitendo cha wachezaji wake kumpiga mwamuzi Israel
Nkongo kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom dhidi ya Azam iliyochezwa Machi 10
mwaka huu.
Pia alimuomba Rais wa TFF, Leodegar Tenga kutoa msamaha wa adhabu ya
kulipa faini iliyotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wawili wa Yanga
ambao mpaka sasa hawajalipa faini hiyo.
Rais Tenga alimshukuru Bhinda kwa ujasiri alioonesha wa kuomba radhi
mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kitendo kile. Aliongeza kuwa kwa
vile yeye ni muumini wa kanuni, na adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa kanuni
hawezi kutoa msamaha, hivyo wachezaji hao walipe faini hizo.
Pia Rais Tenga alisema binafsi haziingilia kamati za TFF katika uamuzi
ambao zinafanya kwa vile zina watu waadilifu, na angekuwa yeye binafsi ndiye
anayetoa adhabu, angetoa adhabu kali zaidi kwa vile vitendo vya kupiga waamuzi
havikubaliki katika mchezo wa mpira wa miguu.
KANUNI ZA NIDHAMU, MAHAKAMA YA USULUHISHI
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais Tenga aliwaambia wajumbe
kuwa Kanuni za Nidhamu (Disciplinary Code) za TFF na uundaji wa Mahakama ya
Usuluhishi (Arbitration Tribunal) ya TFF ambacho ndicho kitakuwa chombo cha juu
cha kutoa haki kwa masuala ya mpira wa miguu nchini vitakamilika mwaka huu.
Pia TFF itaendelea kutafuta wadhamini kwa ajili ya timu za Taifa za
vijana na wanawake, itaendelea kuendesha semina na makongamano katika nyanja
mbalimbali za mpira wa miguu, kutengeneza mtaala wa academy na kutengeneza
mpango wa maendeleo (Comprehensive Plan) baada ya ule wa awali kumalizika mwaka
huu.
No comments:
Post a Comment