BEKI mahiri na Nahodha wa timu ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, Shadrack Nsajigwa 'Fuso', na Abuu Ubwa, wameachwa katika usajili wa Klabu hiyo ya Msimu ujao wa Ligi Kuu.
Habari zilizoufikia mtandao huu wa www.sufianimafoto.blogspot.com, kutoka ndani ya Klabu hiyo zinasema, nyota hao wameachwa kutokana na kushuka viwango.
Mtonyaji wa habari hizi amesema kuwa, kutokana na kushuka kwa kiwango cha uchezaji cha wachezaji hao kuliwafanya washindwe kutoa mchango uliotarajiwa na Klabu na mashabiki wa timu hiyo katika msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara iliyofikia tamati Mei 6, mwaka huu.
Aidha timu ya Yanga iliyo chini ya Kocha wake Mserbia, Kostadin Papic ilimaliza ligi hiyo kwa kushindwa kutetea ubingwa wake, ikiwa nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Azam FC.
Imeelezwa kuwa kutemwa kwa wachezaji hao, ni sehemu ya mkakati kabambe wa kusuka upya Kikosi cha wanajangwani hao kuelekea mbio za kutetea ubingwa wao wa Kombe la Kagame na msimu mpya wa Ligi Kuu ujao.
“Tumedhamiria kuwa na kikosi bora, chenye hari na kasi ya ajabu si bora kuwa na kikosi tu ila 'Kikosi Bora' katika ligi kuu ijayo na michuano mingine, hivyo ndiyo maana tunaanza kusuka upya kikosi chetu kwa kuangalia uwezo wa wachezaji na kupunguza wale ambao uwezo wao umefikia tamati''. kilisema chanzo hicho.
Aidha Klabu hiyo hivia sasa inaendelea na 'Speed 120' ya kusaka nyota wakali wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kuziba nafasi za wale watakaoachwa kwa lengo la kujenga kikosi bora cha ushindani.
Mbali ya Nsajigwa na Ubwa, nyota wengine walio kwenye hati hati ya kuachwa ni pamoja na Shamte Ally, Bakari Mbegu na Kiggi Makasy, ambao wameelezwa ni kutokana na sababu kadhaa, ikiwemo kushuka viwango pia.
Kuachwa kwa Nsajigwa kunakuja huku kukiwa na habari za Yanga kuanza kusaka saini za nyota kadhaa wakiwemo Uhuru Seleman, Juma Jabu na Juma Nyoso kwa lengo la kuimarisha kikosi cha msimu ujao.
Kabla ya kutua Yanga mwaka 2006 akitokea timu ya Moro United, Nsajigwa aliwahi kuichezea Prisons ya Mbeya kwa mafanikio kama ilivyokuwa kwa rafiki yake, kipa Ivo Mapunda aliyehama naye Moro Utd hadi Yanga.
No comments:
Post a Comment