Mhe. Ali Kessy, Mbunge wa Nkasi Kaskazini. |
Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini kupitia CCM, Mhe. Ali Mohamed Kessy, ameng’ara katika shindano maalum la kulenga shabaha kwa matumizi ya bastola na kuwamwaga wapinzani wake, wakiwamo waheshimiwa Mathayo David, Martha Mlata na David Silinde.
Akizungumza bungeni jana, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai alisema kuwa, Mhe. Kessy, alionyesha umahiri mkubwa katika shindano hilo lililowashirikisha waheshimiwa wabunge kwa kulenga shabaha kwa kutumia bastola na bunduki, lililofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki na kuibuka kidedea katika shindano hilo.
Washindi wengine waliotangazwa bungeni jana katika shindano la kulenga shabaha ni pamoja na Waziri wa Ushirika na Masoko, Mhe. David, ambaye yeye aliibuka kidedea katika kutumia bunduki aina ya Sub Machine Gun (SMG) huku Mhe. Mlata akishika nafasi ya pili katika kulenga shabaha kwa kutumia bunduki aina ya Light Machine Gun (LMG).
Wakati Mhe. Ndugai akimtangaza Kessy, kuwa ndiye mshindi katika kulenga shabaha kwa bastola, ukumbi mzima wa bunge uliripuka kwa shangwe, vicheko na nderemo.
Haikufahamika mara moja ni kwanini wabunge walimshangilia sana Kessy, ingawa inaeleweka wazi kuwa mbunge huyo amekuwa maarufu sana kutokana na hoja yake anayoitoa kila mara ya kutaka watu wote wanaothibitika kujihusisha na vitendo vya ufisadi wasionewe huruma na sheria itungwe ya kutaka wauwawe kwa kunyongwa ama kupigwa risasi.
Mhe. Kessy amekuwa akitetea hoja yake hiyo kwa maelezo kuwa vitendo vibaya vya kifisadi katika maeneo mbalimbali husababisha maafa ya watu wengi maskini wasiokuwa na hatia na hivyo, ni vizuri sasa nao wauawe kama inavyofanyika nchini China.
No comments:
Post a Comment