Habari za Punde

*ALIYEMRITHI ROSTAM AZIZ JIMBO LA IGUNGA DKT. DALALI KAFUMU AVULIWA UBUNGE LEO

Habari zilizoufikia mtandao huu hivi punde, zinasema kuwa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, leo imetoa hukumu ya Kesi ya Ubunge iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa Jimbo la Igunga, Dkt. Dalali Peter Kafumu, kupitia Chama cha Mapinduzi CCM na kumvua hadhi hiyo ya Ubunge baada ya mgombea mwenzake wa nafasi hiyo, Joseph Kashindye, kufungua kesi mara tu baada ya uchaguzi wa mwaka 2011.

HABARI KAMILI:-
 Kwa hukumu hiyo sasa, Jimbo la Igunga mkoani Tabora liko wazi kuanzia leo baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora kumvua ubunge Peter Dalay Kafumu wa CCM kufuatia hukumu iliyotolewa leo katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi uliomuweka madarakani mbunge huyo ambayo ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joseph Kashindye.

Taarifa kutoka Tabora zimeeleza kuwa hukumu hiyo iliyovuta hisia za maelfu ya wakazi wa mji huo na maeneo ya jirani, ilisomwa kuanzia mishale ya saa 3:00 asubuhi.

Pamoja na Kafumu, Kashindye pia aliwashitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Protace Mgayane . Shauri hilo lilianza kusikilizwa na Jaji Mary Nsimbo Shangali tangu Machi 26, 2012.

Akizungumza baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Kafumu amesema kuwa hajaridhishwa kwani yeye alichofanya wakati wote wa kampeni ilikuwa ni kunadi sera za chama chake (CCM).

Kafumu aliongeza vile vile kuwa tangu awali, alishaeleza mara kadhaa kuwa haridhishwi na jaji aliyekuwa akisikiliza shauri hilo kwa vile alikuwa akiegemea upande mmoja; na kwamba ndicho alichokifanya leo wakati akitoa hukumu.

Kafumu ambaye kabla ya kujitosa kwenye siasa alikuwa ni Kamishna wa Madini, alisema kuwa uamuzi wote kuhusu nini cha kufanya baada ya uamuzi wa mahakama leo anauacha kwa chama chake (CCM) na kwamba hivi sasa, yeye atarejea katika kazi yake ya utaalam wa madini.

Awali, Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Nzega, Sylvester Kainda, alikaririwa akisema kuwa Mahakama Kuu kanda ya Tabora ilipanga hukumu hiyo isomwe jana lakini kutokana na siku hiyo kuwa Idd Pili, hukumu ikasomwa leo.

Profesa Abdallah Safari ambaye ni wakili wa mlalamikaji Kashindye, alisema kabla ya hukumu kutolewa leo kuwa wamewasilisha malalamiko 13 mahakamani.

Katika kesi hiyo, Kafumu alikuwa akitetewa na mawakili wawili ambao ni Antony Kanyama na Kayaga Kamaliza.

Miongoni mwa malalamiko yaliyotolewa na Kashindye katika kesi hiyo ni pamoja na vitisho katika uchaguzi huo mdogo uliofanyika baada ya kujiuzulu kwa mbunge wa zamani kupitia CCM, Rostam Aziz, mawaziri kutoa ahadi kama ya ujenzi wa daraja la Mbuntu pamoja na ahadi za kugawa mahindi kwa watu waliokuwa wakikabiliwa na njaa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.