Habari za Punde

*PUSH MOBILE KUBORESHA MALIPO YA WANAMUZIKI WA KIBONGO

 Mkurugenzi  Mtendaji  wa kampuni ya Push Mobile Limited, Freddie Manento, akizungumza na wanamuziki na wadau wake waliofika katika mkutano wa kujadili masuala mbali mbali ya biashara ya muziki nchini.
******************************
Na Mwandishi wetu
KAMPUNI ya Push Mobile Limited imeahidi kuboresha  kazi za wanamuziki pamoja na asilimia ya malipo yanayotokana na milio na miito ya simu.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Freddie Manento katika mkutano na wanamuziki na wadau wa muziki uliofanyika kwenye hotel ya Serena.
Manento alisema hayo baada ya kuweka bayana mchakato mzima wa mfumo wa  biashara ya muziki Tanzania katika mkutano uliohudhuria na wasanii zaidi ya 80 wa muziki wa aina tofauti ikiwa kama injili, bongo fleva, muziki wa dansi, taarab na reggae,  hip hop na watayarishaji mbali mbali (producers).
Alisema kuwa kwa sasa Push Mobile inatoa wastani wa asilimia 20 mpaka 40 kwa mwanamuziki pamoja na wadau wao .  Alisema kuwa kiwango hicho hutolewa baada ya wao kupokea kutoka kwa mitandao ya simu kati ya asilimia 35 mpaka 60.
“Lengo letu ni kuona wanamuziki wanafaidika na kazi zao hasa kupitia milio na miito ya simu, biashara ambayo kwa sasa imewaingizia kipato kikubwa wanamuziki baada ya kuanguka kwa soko la mauzo ya albamu e na kutopata kipato chochote kutoka kwenye redio na televisheni kama ilivyoelezwa na  Naibu Waziri wa Mawasiliano , Sayansi na Teknolojia wakati anajibu hoja ya Mbunge wa Chadema, Zitto Kabwe,” alisema Manento.
Alisema kuwa asilimia ngapi wataongeza, itatokana na majadiliano na kampuni za mitandao ya simu na hata kama kampuni hizo zitakataa kuongeza ili kuwafaidisha wasanii, wao wataongeza tu.
Alifafanua kuwa kampuni yao imekuwa ikiingia gharama kubwa za kiuendeshaji katika kupromoti nyimbo za wasanii ili kuweza kupata soko.
“Tunatumia si chini ya milioni  25 kwa mwezi kwa ajili ya kuandaa matangazo na kudhamini vipindi katika redio na televisheni kwa ajili ya kupromoti nyimbo za wasanii ili kuweza kupata masoko, pia tunatumia zaidi ya million 7 kwa kazi ya kutengeneza nyimbo ili ziwezwe kuingizwa katika mifumo mbali mbali ya simu za mikononi,” alisema.
Kuhusiana na kuchelewa kwa malipo ya wanamuziki, Manento alisema kuwa tatizo hilo linatokana na ucheleweshwaji wa wadau husika kufanya malipo kwa wakati.
 “Push imejitahidi kuondoa tatizo hilo kwa kuwalipa wanamuziki kwa fedha zake huku ikiendelea kudai kutoka kwa wadau husika ambao  mara nyingine ukaa miezi sita bila kutulipa, ni changamoto kwetu, lakini tumejitahidi kufikia malengo na kutatua matatizo kwa wasanii, japo changamoto ni kubwa, nawaomba wanamuziki kuelewa tatizo hilo, ” alisema.
Akizungumza katika mkutano huo mtayarishaji maarufu wa muziki nchini,  John Water Sharizo au Man Water aliipongeza Push Mobile kwa jitihada zake za kuinua kipato kwa wanamuziki kwani zamani walikuwa wananyonywa sana katika mauzo ya albamu.
 Man Water alisema kuwa ni jukumu la Push  Mobile ambayo inafanya kazi na wanamuziki  wengi hapa nchini kuhakikisha kuwa wateja wake wanapata  faida na kazi zao kwani wao ndiyo wameingia mikataba na wanamuziki na wala siyo makampuni ya simu.
Alisema kuwa wanashukuru kwa kipato kilichopo kwani hapo awali walikuwa wanachapisha CD au kaseti 200 na kuuzwa mwaka mzima bila kupata mrahaba  kinyume na sasa.
Wanamuziki mbali mbali walihudhuria mkutano huo walifuraishwa sana kwani waliweza kuweka hadharani kero zao mbali mbali na kujibiwa na mkurugenzi huyo na kuridhishwa.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.