Habari za Punde

*YANGA YACHEZEA KICHAPO CHA 3-0 KWA MTIBWA, SIMBA YASHINDA 2-0 DHIDI YA JKT RUVU


TIMU ya Yanga ya jijini Dar es Salaam, leo imepokea kichapo kitakatifu cha mabao 3-0 kutoka kwa wenyeji wao Mtibwa Sugar, katika mchezo wa raundi ya pili ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Katika mchezo wa leo, Yanga ilizidiwa katika kila idara hadi timu hizo zinakwenda mapumziko, tayari Mtibwa Sugar walikuwa wakiongoza kwa mabao 2-0, yaliyofungwa na beki wa kati, Dickson Daudi dakika ya 11 akiunganisha kwa kichwa kona ya beki wa kushoto Malika Ndeule na bao la pili akifunga katika dakika ya 43.

Haruna Niyonzima, alionekana kushindwa kuiongoza vema timu, jambo ambalo lilimfanya kiungo mkabaji Athumani Iddi ‘Chuji’ kupanda mbele zaidi ili kuongeza mashambulizi.

Kipindi cha pili Kocha wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet, alianza kwa kufanya mabadiliko akiwatoa, Frank Damayo na David Luhende na kuwaingiza Simon Msuva na Stefano na Mwasyika, lakini bado ukuta wa Mtibwa ulikuwa mgumu kupitika kiurahisi.

Kocha huyo, Tom, aliendelea kufanya mabadiliko kwa kumtoa beki Mbuyu Twite na kumuingiza na mshambuliaji Didier Kavumbangu, lakini bado upepo haukuwa mzuri kwa upande wao.

Bao la 3, liliwekwa kimiani na Hussein Javu katika dakika ya 86, kwa shuti la mbali, wakitoka kushambuliwa.

Katika dakika ya 89, Hamisi Kiiza alipaisha mkwaju wa penalti, baada ya beki wa Mtibwa, Daudi, kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

YANGA:- Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, , Mbuyu Twite/Kavumbangu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo/Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na David Luhende/Stefano Mwasyika.
MTIBWA SUGAR:- Shaaban Hassan Kado, Malika Ndeule, Issa R Issa, Dickson Daudi, Salvatory Ntebe, Shaaban Nditi, Jamal Mnyate/Babu Ally Seif, Awadh Juma, Hussein Javu, Shaaban Kisiga ‘Malone’ na Vincent Barnabas/Ally Mohamed ‘Gaucho’.
WAKATI HUO HUO:_ Katika mechi nyingine,  Simba SC imeendeleza dozi, baada ya kuichapa JKT Ruvu mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, licha ya kucheza pungufu baada ya Emanuel Okwi kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Mabao ya Simba yalifungwa na viungo Amri Kiemba na Haruna Moshi ‘Boban’ na kwa matokeo hayo, Simba inaendelea kuongoza ligi kwa kufikisha jumla ya pointi 6, baada ya awali kuifunga African Lyon 3-0.  
SIMBA SC:- Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba, Haruna Moshi ‘Boban’, Daniel Akuffo, Mrisho Ngassa na Emanuel Okwi. 
KATIKA michezo mingine, Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza Azam imelazimishwa sare ya 2-2 na wenyeji Toto African.
Uwanja wa Kaitaba Bukoba, wenyeji Kagera Sugar wametoka sare ya 0-0 na JKT Oljoro ya Arusha.
Uwanja wa Sokoine Mbeya, wenyeji Prisons wametoka sare ya 1-1 na Coastal Union ya Tanga.
Uwanja wa Chamazi, African Lyon imeifunga Polisi Morogoro 1-0.
Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Ruvu Shooting imeifunga 2-1 Mgambo JKT. 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.