Na Mwandishi Wetu
HATIMAYE mashabiki sita watakaochuana ili kupata wawili kupitia shindano la kusaka mashabiki bora wa Ligi Kuu ya England, maarufu kama ‘Castle Lager Superfans’, wamejulikana, leo jijini dar es Salaam.
Washindi hao sita wamepatikana kutokana na mchujo mkali kutoka kwa mashabiki 361 waliojitokeza kushiriki shindano hilo linaloendeshwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Castle Lager.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Meneja wa Bia ya Castle Lager, Kabula Nshimo, alisema ilikuwa ni mchujo mgumu, kutokana na wingi wa mashabiki waliojitokeza.
Kabula, alisema kuwa miongoni mwa hao sita, watapatikana wawili ambao ndio watakaoungana na mashabiki kutoka nchi nyingine kuunda timu ya ushangiliaji katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika, zitakazofanyika Afrika Kusini mwakani.
Aliwataja mashabiki hao sita na mikoa wanayotoka ikiwa kwenye mabano kuwa ni, Stephen Chuma , John Mosha, Filbert Nestory (Dar es Salaam), Charles Mbaza (Arusha), Denis Mlowe (Iringa) na Yahaya Hamza (Mwanza).
Castle Lager ambao pia ni wadhamini wenza wa Ligi Kuu ya England, itawatembeza mashabiki hao mikoa yote ili kuomba kura, pia kupitia promosheni mbalimbali zitakazoendeshwa nchi nzima.
Kabula alisema, mashabiki 361 walijitokeza kwa kutuma picha zao katika mtandao wa kijamii wa Facebook na promosheni walizoziendesha katika mikoa mbalimbali.
Meneja huyo alisema, baada ya mchujo walipatikana washindi 32 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Iringa, Shinyanga, Mwanza, Arusha na Kilimanjaro, ambao walipigiwa kura na kupatikana 15.
“Katika hao 15 ndio ambao walifanyiwa mahojiano ya ana kwa ana, hivyo wamechujwa na kupatikana sita, ambapo watasakwa washindi wawili ili waunde timu ya Castle Lager Superfans Tanzania,” alisema.
Kabula alisema washindi hao wawili watakaopatikana, wataungana na wengine kutoka Swaziland, Zambia, Afrika Kusini na Zimbabwe ili kuunda timu ya ushangiliaji itakayogharamiwa kila kitu katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika hapo mwakani. Fainali hizo zitafanyika Afrika Kusini.
Mashabiki hao sita unaweza kuwapigia kura kwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno ukitaja jina la mshiriki kwenda namba 0683 536631.
No comments:
Post a Comment