NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
KAMATI ya Bunge ya Hesabu za Serikali(PAC) imetaka Wizara ya Maji kuhakikisha kuwa inaziagiza mamlaka zote na maji zinadhibiti kiwango cha upotevu wa maji ili kuweza kuepushia serikali hasara fedha na wananchi kupata huduma hiyo katika kipindi cha miezi sita.
Kauli hiyo imetolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Zainabu Vullu , ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa kamati hiyo wakati alipozungumza na baadhi ya viongozi wa wizara hiyo, mamlaka na taasisi za maji kuhusu ripoti ya ukaguzi na ufanisi wa utendaji kazi wa wizara hiyo.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema hayo kufuatia ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuonesha kuwa serikali imepata hasara ya sh. bilioni 92.9 kutokana na tatizo la upotevu wa maji katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2007/2008 hadi 2009/2010.
Mwenyekiti huyo aliitaka wizara hiyo kuelezea ni sababu zipi zimeisababisha serikali kupata hasara ya fedha hizo.
Akijibu swali hilo Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Christopher Sayi alisema ni kweli kumekuwa na upotevu wa maji katika miji , hali hiyo imetokana na historia kuwa miundombinu haijakarabatiwa na imechakaa na hakuna uwekezaji katika sekta ya maji tangu wakati wa Uhuru.
Hata hivyo alisema serikali imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali kuwa tatizo lingine ni ukosefu wa fedha za kutosha na wafanyakazi.
Aidha kamati hiyo imeitaka Hazina isikie kilio cha wizara hiyo cha kuweza kupatiwa fedha za kutosha katika bajeti yao kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya maji.
Akizungumzia kuhusu upotevu huo, Mkurugenzi wa Huduma za Maji Mijini, Yohana Monjesa alisema ulikuwa katika kiwango cha asilimia 70 lakini sasa kiko asilimia 35 mji yote nchi nzima. Alisema kiwango cha kimataifa cha upotevu huo kinatakiwa kiwe asilimia 20.
Alisema wizara hiyo inafanya juhudi ili iweze kufikia kiwango hicho cha kimataifa.
Mwenyekiti huyo pia, alisema ripoti hiyo imeonesha kuwa asilimia 60 za mita za ankra za maji jijini Dar es Salaam hazisomwi , katika ripoti ya mwaka 2009/2012 alihoji tatizo linasababishwa na nini?
Akijibu swali hilo , Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji safi na Maji taka(DAWASCO), Jacson Midala tatizo hilo limetokana kuonngezeka kwa mita nyingi , ambapo mwaka 2005 ni asilimia 35 za mita zilifungwa tofauti na sasa zimefikia asilimia 94 na kuwa mzigo kwa wasomaji.
Midala alisema ili kutatua tatizo hilo wanabadili mfumo wa usomaji mita kwa kuwekeza kwa kutumia vifaa vya kisasa na utaratibu huo utaanza kutumika mwishoni mwa wezi Novemba mwaka huu.
Hata hivyo alisema usomaji wa mita sasa ni asilimia 92 katika jiji hilo.
Akifafanua suala hilo ,Midala aliongeza kuwa kifaa hicho cha kisasa kiitwacho Digital Data Logger kiko kama simu ya mkononi kitakuwa na uwezo wa kusoma mita 300 kwa siku hivyo kitasaidia ulipaji wa ankra sahihi za huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment