Habari za Punde

*BUKOBA VETERANS YAANDAA MASHABIKI 60 KUTOKA KANDA YA ZIWA KWENDA KUISHANGILIA KIIMANJARO STARS UGANDA-CHALLENGE CUP


PRESS RELEASE
Bukoba Veteran Sports Club ni umoja wa wanamichezo waliowahi kucheza klabu mbalimbali zikiwemo za Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara maskani yake yakiwa mjini Bukoba, Kagera. 

Katika kuhamasisha ushiriki wa timu za Tanzania, Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes, kwenye michuano ya Kombe la Chalenji inayofanyika jijini Kampala Uganda, Bukoba Veteran imeandaa safari ya mashabiki walioko mkoa wa Kagera na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwenda kushangilia mechi za timu hizo.


Kwa kuanzia, mashabiki hao wataondoka mjini Bukoba Jumapili Novemba 25, 2012 kwenda kuishangilia timu ya taifa ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars katika mechi yake ya kwanza ya michuano hiyo dhidi ya Sudan Kaskazini.


Nia na madhumuni ya safari hiyo ni kuhamasisha wachezaji wa timu za taifa za Tanzania waweze kufanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kutoa hamasa kwa watanzania kujenga tabia ya kushangilia timu zao. Pia tunadhani kuwa ushiriki wetu utaongeza ushindani katika michuano hiyo.

Tayari taratibu zote zimeshafanyika ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ili wawasiliane na mamlaka zinazohusika kwa ajili ya kupatiwa eneo maalumu uwanjani litakalowezesha watanzania waweze kuishangilia vizuri timu ya taifa. 

Tunatarajia kwenda uwanjani na zaidi ya mashabiki 60 ambao hivi sasa wanakamilisha taratibu za mwisho za kuvuka mpaka wa nchi.

Matarajio yetu ni kuendelea kuziunga mkono timu za taifa katika michuano hiyo hadi kufikia mwisho wa michuano. Tunaomba watanzania wengine walioko kanda ya ziwa katika mikoa ya Shinyanga, Mara na Mwanza watuunge mkono  Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Imetolewa na
Shija Richard
 Katibu Mkuu wa Bukoba Veteran 

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.