TENGA ATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU TFF
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Leodegar Tenga ambaye ndiye Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho hilo tayari
ametoa notisi ya mkutano huo utakaofanyika Februari 23 na 24 mwakani jijini Dar
es Salaam.
Mkutano huo utafanyika Februari 23 mwakani na kufuatiwa
na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata. Ajenda ya uchaguzi iko chini ya Kamati ya
Uchaguzi ya TFF.
Notisi hiyo imetumwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu ambao
ni kutoka vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki, klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.
Ajenda za Mkutano Mkuu zitatumwa kwa wajumbe siku 15
kabla ya mkutano huo wenye wajumbe zaidi ya 100.
NUSU FAINALI UHAI CUP KUPIGWA KARUME
Mechi za nusu fainali ya michuano ya Kombe la Uhai 2012
inayoshirikisha timu za vijana wenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom zitachezwa kesho (Desemba 21 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu
ya Karume, Dar es Salaam.
Nusu fainali ya kwanza ya michuano hiyo inayodhaminiwa
na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai itazikutanisha timu za
Mtibwa Sugar ya Morogoro na Azam na itafanyika kuanzia saa 2 kamili
asubuhi.
Simba na Coastal Union zitacheza nusu fainali ya pili
kuanzia saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo. Mtibwa Sugar imepata tiketi
ya nusu fainali baada ya kuichapa African Lyon mabao 3-1 wakati Simba iliilaza
Oljoro JKT mabao 2-0.
Nayo Azam iliindoa JKT Ruvu kwenye robo fainali kwa bao
1-0 huku Coastal Union ikipata ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ruvu Shooting
kwenye mechi ya mwisho ya robo fainali.
Mechi ya fainali na ile ya kutafuta mshindi wa tatu
zitachezwa Jumapili (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Dar es Salaam. Mechi ya mshindi wa tatu itaanza saa 2 kamili asubuhi
wakati ya fainali itakuwa saa 10 kamili jioni.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA TWFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaupongeza
uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA)
uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Desemba 19 mwaka huu) hoteli ya
Midlands mjini Morogoro.
Ushindi aliopata Lina Kessy aliyechaguliwa tena kuwa
Mwenyekiti pamoja na wajumbe wengine wa Kamati ya Utendaji unaonesha jinsi
ambavyo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TWFA walivyo na imani kwao.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya TWFA, na kwamba ina changamoto kubwa ya kuhakikisha inaendesha
shughuli za chama hicho kwa kuzingatia katiba na kanuni.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA chini
ya Mama Ombeni Zavala na Kamati ya Uchaguzi ya TFF inayoongozwa na Deogratias
Lyatto kwa kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa utulivu na kwa kuzingatia
Katiba ya TWFA na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Safu mpya ya uongozi wa DRFA inaundwa na Lina Kessy
(Mwenyekiti), Rose Kissiwa (Makamu Mwenyekiti), Amina Karuma (Katibu), Zena
Chande (Mwakilishi wa Mkutano Mkuu wa TFF) wakati mjumbe wa Kamati ya Utendaji
ni Triphonia Temba.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF)
No comments:
Post a Comment