Habari za Punde

*SERIKALI MKOANI KAGERA YATOA MIKOPO YA ZAIDI YA SH. MILIONI 83 KWA VIKUNDI VYA VIJANA


Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
SERIKALI Mkoani Kagera imevikopesha vikundi  mbalimbali vya maendeleo vya vijana kupitia Vyama Vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) zaidi ya shilingi milioni 83 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ili kuwawezesha vijana waweze  kujiajiri wenyewe na kujikwamua  kiuchumi .
Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa huo Kanali Mstaafu Fabian Massawe wakati akisoma taarifa fupi ya mkoa  kwa  Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara aliyepo mkoani humo kwa ajili ya kuangalia jinsi  fedha za mkopo kutoka mfuko wa vijana  zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha.
Kanali Mstaafu Massawe alisema kuwa Serikali  inasimamia utekelezaji wa sera ya maendeleo ya vijana kwa kuratibu shughuli za mifuko ya vijana na kufuatilia utoaji na urejeshaji wa mikopo, kuhamasisha vijana na kufufua moyo wa kujitolea na kukuza na kuendeleza vipaji mbalimbali walivyonavyo vijana ili kuwawezesha kujiajiri kupitia mafunzo yanayohusu stadi za kazi na maisha
“Changamoto tunazokabiliana  nazo katika kuwakopesha vijana ni mahitaji makubwa ya mkopo ukilinganisha na uwezo wa SACCOS au wakopeshaji wengine, urejeshaji hafifu wa mikopo kutoka kwa wakopaji, ukosefu wa ajira, uvivu na uzurulaji, vijana kutaka mafanikio kwa haraka na matumizi ya madawa ya kulevya kwa baadhi ya vijana”, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aliendelea kusema kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo Serikali ngazi ya mkoa inafuatilia kwa karibu ili kuona kwamba matamko ya sera ya Taifa ya Maendeleo ya vijana yanazingatiwa na kuingizwa katika  maendeleo ya Halmashauri lengo kuu ni mkoa kuwa na vijana wenye ari ya kuwajibika na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii, wazalendo, wenye maadili na kupenda nchi yao.
Kwa upande wake waziri Dk. Mukangara alisema kuwa hivi sasa Serikali inaangalia uwezekano wa kuongea mkopo kwa SACCOS zinazolenga shughuli za maendeleo ya vijana  kutoka shilingi milioni tano hadi kumi kwani mahitaji ni makubwa na hayakidhi haja.
Dk. Mukangara alisema kuwa vijana  watumie fursa zinazowazunguka na kutambua kwamba ni wajibu wao na siyo jukumu la wazazi kuwakumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwani ni aibu kijana kula chakula  bila ya kukitolea jasho huku mzazi akihangaika kufanya kazi.
“Vijana watambue kuwa fursa ya kupata ajira  ipo katika kero zinazowazunguka hivyo basi uongozi wa Serikali mkoani humu uwahamasishe vijana ili waweze kujiajiri na kuajiri kwani maendeleo ya Kagera yanawategemea wao hakuna mtu mwingine atakayeleta maendeleo yao”, alisema Waziri Dk. Mukangara.
Alimalizia kwa kuwataka viongoziwa Serikali kuwafuatilia vijana kwa ukaribu katika Kata na kuweza kuwafundisha na kuwashirikisha  katika miradi ya maendeleo ili waweze kusaidiana na jamii inayowazunguka kwa kushiriki ulinzi shirikishi, kupambana na tatizo la uhamiaji haramu na kufahamu umuhimu wa  utii wa sheria.
Mkoa wa Kagera unakadiriwa kuwa na idadi ya watu 2,739,492 kati ya hao wanawake 1,386,669 na wanaume 1,353,123 ambapo vijana ni 903,608 wenye umri wa miaka 15 hadi 35 sawa na asilimia 33 ya wakazi wote ambapo  kati ya hao wa kike ni 459,867 na wa kiume 443,741.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.