Habari za Punde

*SERIKALI YA ZANZIBAR KUENDELEA KUIMARISHA SEKTA ZA KIUCHUMI

 Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Pandu Ameir Kificho (wa pili) akiwa na wapambe wake akitoka nje ya Ukumbi wa Baraza hilo mara baada ya kuahirisha Mkutano wa Kumi wa Baraza la wawakilishi Zanzibar, jana.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akizungumza na Mwakilishi wa Viti Maalum CUF (katikati) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Zahra Ali Hamadi, na (kulia) yake ni Mh. Shawana Bukheit Hassan Mwakilishi wa Jimbo la Dole.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa pia ni Mkuu wa Shughuli za Serikali Balozi Seif Ali Iddi, akitoa Hotuiba ya ufungaji wa Mkutano wa Kumi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar lililofanyika katika Ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha na Hassan Issa wa –OMPR – ZNZ
*******************************
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na jitihada za kuimarisha sekta za Kiuchumi na Ustawi wa Jamii lengo kuu likiwa lile lile la kukuza Uchumi na kupunguza umaskini miongoni mwa Wananachi walio wengio hapa Nchini.
Kauli hiyo im etolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akiufunga Mkutano wa Kumi wa Baraza la Wawakilishi Zanzib ar  uliokuwa ukifanyika katika ukumbi wa Baraza hilo uliopo Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
 Balozi Seif alisema jitihada hizi muhimu zitafanikiwa vyema endapo wananchi wote kwa kushirikiana na viongozi wao watakubali kuwajibika kikamilifu  na baadhi yao kuwacha tabia za kuchafua mazingira sambamba na uharibifu wa miundo mbinu ambayo Serikali Kuu tayari imeshaiweka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenye muundo wa Umoja wa Kitaifa ikiongozwa na Rais wake Dr. Ali Mohd Sheni inafanya kazi kubwa ya kuwaletea Maendeleo Wananchi wake.
“ Katika kufanikisha hayo Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya Elimu, afya, Biashara na Viwanda, Kilimo, Mifugo na Uvuvi, miundo mbinu na kuhakikisha  wananchi wote Mijini na Vijijini wanapata Maji safi na salama kwa kuimarisha  Afya zao”. Alifafanua Balozi Seif.
Akizungumzia suala la sheria zinazotungwa na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa nia ya kuwatumikia Wananchi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  aliwanasihi watekelezaji wa sheria hizo wazisimamie na kuhakikisha  kuwa zinatekelezwa ipasavyo bila ya kumuonea haya au aibu mtu ye yote atakayezikiuka sheria hizo.
Alisema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamekuwa wakilalamikia kuwa sheria nyingi zimetungwa lakini  kumekuwa na udhaifu wa kusimamia utekelezaji wake.
Aliiitolea mfano sheria ya usimamizi wa usalama Bara barani ambayo jamii imekuwa ikishuhudia waendesha baskeli wanatumia vyombo vyao hasa usiku bila ya taa wakati baadhi ya madereva  huendesha gari bila ya nambari ambapo haijuilikani madhumuni yao kufanya hivyo.
Balozi Seif aliipongeza Teule ya Baraza la Wawakilishi iliyoundwa kuchunguza utendaji wa shirika la Umeme Zanzibar na Kamati Teule ya kuchuguza utendaji wa Baraza la Manispaa kwa umakini wao na kufanya uchunguzi wa kina kuhusu utendaji katika Taasisi hizo mbili.
Alisema Serikali imezipokea Ripoti hizo za Kamati Teule zilizowasilishwa  katika Baraza la Wawakilishi na itazifanyia kazi Taarifa hizo pamoja na mapendekezo yake kwa umakini  mkubwa na kuchukuwa hatua kadri itakavyoonekana inafaa.
Balozi Seif aliwahakikishia Wajumbe wa Baraza hilo kwamba wale wote waliotajwa kwenye ripoti hizo watashughulikiwa  ipasavyo kwa kuzingatia haki na Utawala Bora kama baadhi ya Wajumbe hao walivyoshauri.
Kuhusu suala la Ununuzi wa Meli kubwa kwa ajili ya usafiri wa uhakika wa Wananachi wa Zanzibar na Mwambao wa Afrika Mashariki Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema  Serikali  inatarajiwa kutiliana saini Mkataba   na Kampuni ya  Damen Kutoka Nchini Uholanzi  kwa ajili ya ujenzi wa Meli Mpya ya abiria na Mizigo.
Balozi Seif alisema Meli hiyo itakayokuwa na uwezo wa kuchukuwa Abiria 1,200 na Tani 200 za Mizigo inatarajiwa kuchukuwa miezi 18 utengenezaji wake  mara baada ya mkataba huo kutiwa saini.
“ Wananchi wa Zanzibar wategemee  kama mambo yote yatakwenda sawa, kupata meli mpya mnamo robo ya mwisho wa mwaka 2014, ingawa inawezekana ikawa zaidi kabla ya hapo”. Alifafanua Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza la wawakilishi  walijadili na kupitisha Miswaada mine ya sheria pamoja na Mawaziri kujibu  maswali ya wajumbe wa Baraza hilo yapatayo 72.
Miswaada hiyo ni  Mswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya ruzuku kwa vyama vya siasa nambari 6 ya mwaka 1997 pamoja na Mswada wa sheria ya marekebisho ya usafiri nambari 5 ya mwaka 2006.
Mengine ni Mswada  wa sheria ya kuanzisha shirika la Utangazaji Zanzibar, Kazi, Majukumu na Utawala wake  pamoja na mambo mengine yanayohusiana na hayo na Mswada wa sheria ya kuanzishwa kwa shirika la Meli Zanzibar kazi, Uwezo na Mambo mengine yanayohusiana na hayo.
Baraza la Wawakilishi Zanzibar limeahirishwa hadi Jumatano ya Tarehe 3 Aprili mwaka 2013 saa 3.00 za asubuhi.
 Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
29/1/2013.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.