Habari za Punde

*MBEZI VETERANS YAIKACHA KIJITONYAMA VETERANS


Mratibu wa timu ya Kijitonyama Veterans, Majuto Omary akimtoka mchezaji wa timu ya Kombaini ya Tabora, Ibrahim Masoud “Maestro” katika moja ya mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye uwanja wa Kijitonyama. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 huku mabao yakifungwa na wachezaji hao wawili kwa upande wa timu zao.
**********************************
Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa timu ya Kijitonyama Veterans umepitisha azimio la kutocheza mechi  yoyote ya kirafiki dhidi ya timu ya Mbezi Veterans  ya barabara ya Morogoro kutokana na kile ilichokiita ‘tabia si ya kiwanamichezo’.

Kauli hiyo ilitolewa na mratibu mkuu wa timu hiyo, Majuto Omary kufuatia kitendo cha timu hiyo kushindwa kutokea uwanjani katika mchezo wao maalum wa kirafiki uliopangwa kufanyika jana asubuhi kwenye uwanja wa  Kijitonyama.

Majuto alisema kuwa mechi hiyo iliombwa na timu hiyo ya Mbezi  na wao (Kijitonyama) kuwakubalia kutokana na ukweli kuwa michezo ni afya mbali ya kudumisha urafiki.

Alisema kuwa  mechi hiyo ilipangwa kuanza saa 2.00 asubuhi, na timu hiyo ilithibitisha nusu saa kabla ya mechi hiyo kuwa wanakuja na wapo katika maandalizi.

Alifafanua kuwa baada ya hapo, viongozi wa timu hiyo hawakuonekana uwanjani na mbaya zaidi hawakupokea simu zao  walizokuwa wanapiga ili kujua wamefikia  wapi. 

“Kinanchosikitisha ni kwamba, walituweka hapo uwanjani na mbali ya kuwatumia ujumbe wa simu ya mkononi kuwa wamefika wapi au wamekwama, hawakujibu chochote, hii inaonekana kuwa ni makusudi,” alisema Majuto.

Majuto ambaye pia ni kiongozi wa timu ya waandishi wa habari za michezo nchini (Taswa FC), alisema kuwa hiyo si mara ya kwanza kwa timu hiyo kushindwa kutokea uwanjani bila ya kutoa taarifa.

“Waliwahi kuomba kucheza na Taswa FC pale Leaders Club, tukawakubalia, lakini hawakutokea uwanjani na hata simu zetu wakawa hawapokei wala kujibu ujumbe kusema kuwa wameshindwa kuja, walituacha uwanjani na kupoteza muda, hii ni tabia yao,” alisema.

Alisema kuwa haya maamuzi ni ya kudumu na watajaribu kuzitahadharisha na timu nyingine kuhusiana na vitendo vya timu hiyo  kwani  ni vya kupotezea muda wanamichezo.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.