Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia, jana jioni kuhudhuria utiwaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).PICHA NA IKULU
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amewasili
Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 23, 2013 kuhudhuria utiwaji saini Mpango wa
Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mpango
huo unatarajiwa kutiwa saini kesho Februari 24, 2013 na Wakuu wa Nchi kutoka Ukanda
wa Maziwa Makuu, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya
Burundi, Jamhuri ya Kongo (Brazaville), Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania pamoja na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Aidha,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya
Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma, pamoja na wenyeviti wa Jumuiya
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR)
watatia saini Mpango huo kama mashahidi na wadhamini.
Mpango
huo una nia ya kuchangia juhudi ambazo zimefanywa na Ukanda wa Maziwa Makuu
(ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini
mwa Afrika (SADC) katika kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda wote wa
Maziwa Makuu kwa ujumla.
Mpango
huo pia umetilia maanani mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya mashauriano
kati ya wakuu wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo
ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Imetolewa na:
Muhidin
Issa Michuzi,
Mwandishi
wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu,
DAR
ES SALAAM.
23
Februari, 2013
No comments:
Post a Comment