Habari za Punde

*WAKAZI WA WILAYA YA LINDI MJINI WATAKIWA KUJIUNGA NA HUDUMA YA MFUKO WA AFYA YA JAMII


Mjumbe wa NEC, Lindi mjini, Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kineng'ena Kata ya Chakonji akiwa katika ziara ya kuwashukuru wanachama kwa kumchagua u-NEC, kukagua na kuimarisha uhai wa Chama wilaya ya Lindi, leo.
 Baadhi ya Kina mama wa Kijiji cha Kineng'ene wakifuatilia kwa makini hotuba ya Mama Salma alipowahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho, akiwa katika ziara ya kuwashukuru wanachama kwa kumchagua u-NEC, kukagua na kuimarisha uhai wa Chama wilaya ya Lindi, leo.
 Mjumbe wa NEC, Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, akimsalimia, Fatuma Mohamed, ambaye ni Mama yake mdogo, alipopita katika kijiji cha Nanyanje, akiwa katika ziara ya kuwashukuru wanachama kwa kumchagua u-NEC, kukagua na kuimarisha uhai wa Chama wilaya ya Lindi, leo.Katikati ni Hamis Marobona, mume wa Fatuma.
Mjumbe wa NEC, Lindi mjini, Mama Salma Kikwete akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kineng'ena Kata ya Chakonji akiwa katika ziara ya kuwashukuru wanachama kwa kumchagua u-NEC, kukagua na kuimarisha uhai wa Chama wilaya ya Lindi, leo. Picha na Bashir Nkoromo
***********************************************
Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
 MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wakazi wa kijiji cha Kineng’ene kata ya Mtanda wilaya ya Lindi mjini kujiunga na huduma ya mfuko wa afya ya jamii (CHF) unaotolewa na Mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF)   ili waweze kuepukana na gharama za matibabu za mara kwa mara wanazolipa pindi wanapougua wakati ambao hawana fedha.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) taifa (NEC) toka wilaya hiyo aliyasema hayo jana alipokuwa akijibu swali la mkazi wa kijiji hicho Sophia Lihame kuhusiana na gharama za upatikanaji wa huduma ya afya wanazolipa kwenye mkutano wa hadhara  wa chama hicho uliofanyika katika kijijini hicho.
 Alisema kuwa gharama ya kujiunga na mfuko wa afya ya jamii  ambayo katika wilaya hiyo inajulikana kama tiba kwa kadi si kubwa ukilinganisha na huduma inayotolewa kwani  familia ya watu sita  inachangia shilingi 10000 katika halmashauri ya wilaya fedha ambayo inatumika kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Mjumbe huyo wa NEC pia aliwataka wakazi wa kata hiyo kutoogopa kupima afya zao ili waweze kujua kama wamepata maambukizi ya Virusi vya Ugonjwa wa Ukimwi (VVU) au la kwani kwa kufanya hivyo kutawawezesha kulinda kinga za miili yao.
Mama Kikwete alisema,  “Kwa wale waliopata maambukizi ya VVU  wasione aibu kujitangaza hadharani kwani ugonjwa huu hauuwi haraka kama maralia pia msiwanyanyapae watu wanaoishi na VVU  kwani wenzenu wamepima na uzijua afya zao tofauti na nyinyi ambao hamjapima”.
Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wananchi hao ambao ni wakulima wadogowadogo kufuata taratibu na  kujiunga katika vikundi vya maendeleo ambavyo vitawawezesha  kupata   mkopo benki na hivyo kujikwamua  na hali ngumu ya maisha na kuachana na dhana kuwa wakulima wadogowadogo hawakopesheki.
 Kwa upande wake Meya wa wilaya hiyo Frank Magali alisema kuwa kutokana na tatizo la upugufu wa chakula katika wilaya hiyo Serikali imetoa  tani 172 za chakula ambazo zitawasili baada ya mbili na kugawiwa bure kwa wazee na watu wasiojiweza ambapo wananchi wa kawaida watauziwa kwa bei naafuu.
Katika Mkutano huo wananchi  walipata nafasi ya kuuliza  maswali mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutaka kujua jinsi Serikali itakavyowasadia ili aweze kulipwa malipo ya pili ya korosho ya shilingi 600 kwa kilo, jinsi gani wakulima wadogo wadogowadogo wanaweza kupata mikopo, upatikanaji wa huduma za afya, upungufu  wa chakula  na upungufu wa walimu hasa wa shule ya msingi kwani shule ya msingi Kineng’ene ina walimu tisa wanaofundisha wanafunzi 640.
Mama Kikwete yuko katika ziara ya kichama ya siku saba katika wilaya ya Lindi mjini atatembelea   kata zote 18 za wilaya hiyo kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mjumbe wa NEC.

No comments:

Post a Comment

SUFIANIMAFOTO Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.